KWA SIMBA HII YANI NI 'JAZA UJAZWE'
UKIHESABU mchezaji mmoja mmoja, Simba inaweza kuwa ndiyo timu iliyosajili wachezaji maarufu na wenye uzoefu mkubwa kuliko timu nyingine za Ligi Kuu Bara msimu huu.
Imeachana na wachezaji kumi na kusajili wengine 14 kutoka nje na ndani ya Tanzania.
Baadhi ya mastaa waliosajiliwa ni pamoja na Mganda Emmanuel Okwi ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa Msimbazi, John Bocco, Shomari Kapombe, Ally Shomary, Aishi Manula na Said Mohammed ‘Nduda’.
“Kiujumla usajili tulioufanya ni mzuri na viongozi wamefanikiwa kuniletea aina ya wachezaji ninaowahitaji ili timu iweze kufanya vizuri msimu unaotarajiwa kuanza hivi karibuni,” anasema kocha wa timu hiyo Mcameroon Joseph Omog.
“Nimepata kundi kubwa la wachezaji wazoefu, waliopevuka na wenye kiwango kizuri, ambao bila shaka watakuwa na mchango mkubwa kwa timu katika mashindano mbalimbali ambayo tutashiriki msimu ujao.
“Matarajio yetu ni kufanya vizuri ambako si kwa namna nyingine bali kutwaa ubingwa kwenye kila mashindano ambayo tutashiriki. Kiu ya mashabiki na kila mmoja ni kutaka kuona timu inapata mafanikio ya kuchukua kombe na si vinginevyo. Msimu uliopita tulifanikiwa kuchukua Kombe la FA tu lakini hatukufanikiwa kubeba lile la Ligi Kuu.
“Kwa ubora wa kikosi cha Simba hivi sasa, kipaumbele cha kwanza ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ambao hatujafanikiwa kuuchukua kwa kipindi kirefu, pia tumepanga kutetea ubingwa wa Kombe la FA sambamba na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.
“Kambi zote mbili (Afrika Kusini na Unguja) zimekuwa na mafanikio kwetu kwa sababu utulivu uliokuwepo umewasaidia wachezaji kuelekeza akili zaidi kwenye programu za mazoezi na kuwa sawa kisaikolojia, jambo ambalo litakuwa na faida kwa timu.
“Kupitia kambi hizo tumepata nafasi ya kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza msimu uliopita, hivyo naamini tutaingia kwenye ligi tukiwa tayari kuikabili vita iliyo mbele yetu.
“Ligi itakuwa ngumu kwa sababu nimesikia timu nyingi zikifanya usajili mzuri na kuanza maandalizi mapema. Na ugumu huo hasa utakuwa kwetu kwa sababu timu nyingi zimekuwa zikikamia sana pindi zinapokutana na Simba na ukiongeza na huu usajili tulioufanya, tutakuwa na vita kubwa.”
Yanga na Kimataifa
Akiwazungumzia wapinzani wake wakubwa hao, Omog anasema:
“Yanga ni timu nzuri ambayo kikosi chake hakijafanyiwa mabadiliko makubwa, hivyo naamini watakuwa tishio. “Nimekuwa nikifuatilia mechi zao, kikubwa kinachowabeba ni kuwa na wachezaji wanaojituma na wenye nidhamu ya kupambana na kufuata maelekezo kwa muda wote wa mechi.
“Ukiwa na timu yenye wachezaji wanaojituma na kujitambua inakuwa ni faida kwa timu jambo ambalo linawasaidia Yanga. Hata hivyo siwaogopi, nawaheshimu kama ninavyoziheshimu timu zote zilizo Ligi Kuu.
“Kuna miezi sita imebaki kabla ya kuanza kwa mashindano ya Afrika kwa ngazi ya klabu, hivyo ni mapema mno kuanza kuzungumzia mashindano hayo wakati kuna ligi na Kombe la FA ambayo tunatakiwa kufanya vizuri.
“Hata hivyo kama nilivyosema awali kwamba mkakati wetu ni kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye kila mashindano.
“Hili litatimia tu iwapo wachezaji watakuwa na nidhamu, juhudi na malengo.”
No comments