JACOB ZUMA AKIRI KUNUSURIKA KULA CHAKULA CHENYE SUMU
KATIKA hali isiyo ya kawaida Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, amedai kwamba kumekuwapo na jaribio la kutaka kumuua kwa sumu kwa kumtumia mtu wake wa karibu mno.
Zuma ameibua madai hayo huku uvumi unaohusisha jina la mmoja wa wake zake ukisambaa ingawa yeye binafsi, licha ya kuthibitisha kuwapo kwa jaribio hilo, amekwepa kutaja moja kwa moja jina la muhusika. Mkewe anayetajwa kuhusishwa katika njama hizo Nompumelelo Ntuli Zuma maarufu kwa jina la “Ma Ntuli” ambaye ni mke wa pili wa kiongozi huyo ambaye hivi karibuni alinusurika kung’olewa katika kiti cha urais baada ya kura alizopigiwa za kutokuwa na imani naye bungeni kutotosha.
“Nusura nife kwa sababu waliniwekea sumu, walifanikiwa kumpa mtu aliyekuwa karibu mno nami na hili nalijua fika,” alidai Zuma bila ya kutaja huyu muhusika katika tukio hilo.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo mwenye kupenda kuendeleza utamaduni mashuhuri barani Afrika wa kuoa wake wengi, amenusurika kuuawa kwa kuwekewa kiwango kikubwa cha sumu kiasi cha kuwashangaza hata baadhi ya madaktari juu ya namna alivyonusurika kifo.
“Mtu waliyemtumia kufanikisha mpango wao ni mtu mwema sana,” alisema Zuma na kusisitiza ya kuwa hata kama watu wanamdhihaki na kumkosoa, anajua kwamba atakufa akiwa tayari amekwishatambua kuwa jambo gani hasa linatibua vuguvugu la ukombozi.
Akizungumza katika mkutano kati yake na makada wa chama tawala cha Afrika Kusini – African National Congress (ANC), mkutano uliofanyika katika Jimbo la Free State hivi karibuni, Zuma aliwaeleza makada hao kwamba alikuwa akijua vuguvugu la ukombozi limeingiliwa kwa kutumia njama mbalimbali ili hatimaye kumng’oa madarakani, jambo ambalo lingevuruga rekodi ya ANC.
Katika mkutano huo uliofanyika Jumamosi iliyopita Zuma aliruhusu kuulizwa maswali kutoka kwa makada hao wa chama hicho, na mengi ya maswali hayo yakilenga tukio la hivi karibuni la kunusurika kwake kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye katika bunge la nchi hiyo wiki iliyopita.
Zuma aliwaambia wanachama hao wa ANC kwamba alipokea simu nyingi baada ya jaribio hilo la kutaka kumng’oa kufeli.
“Nimepigiwa simu kadhaa mara tu baada ya matokeo ya kura kutangazwa, dunia zima ilielekeza macho kwetu,” alisema Zuma akishiria hali ya kutoridhishwa na hatua hiyo ya kumtilia shaka kiasi cha baadhi ya makada wa ANC kushabikia dhidi yake.
Rais huyo alisema ANC ni lazima ijiulize ni kwa nini hasa hoja ya kura ya kutokuwa na imani naye imepata msukumo mkubwa nyakati hizi na vile vile akahoji ni masilahi gani yangeweza kupatikana kwa chama chake endapo angeenguliwa kutoka Ikulu.
“Kuna suala la umoja katika mshikamano wetu, kuna mtu aliwahi kuwaza kwamba siku moja hali itakuwa hivyo? Hakuna. Kwa nini? Siku moja ikitokea hawa jamaa zetu (wanahabari) hawapo nitawaeleza kwa ufasaha,” alisema Zuma akiwalenga wanahabari kwamba hawezi kuweka wazi mambo yote kutokana na wanataaluma hao.
“Ukianza kuwaza kiwango cha fedha kilichotumika kudhoofisha nchi yetu hautaamini,” alizidi kudai Zuma bila kutoa ufafanuzi zaidi.
Kwa mujibu wa Zuma, kiwango cha fedha kilichotumika kimefanikisha kubadili mwenendo wa baadhi ya makada kinyume na namna alivyokuwa akiwafahamu.
“Mapinduzi yetu yameingiliwa, yamehujumiwa,” alisema na kuongeza; “Najua tumevamiwa, bila kujali kwa namna gani watu hao ni werevu, natambua kwamba na kwa kweli, mara kwa mara, nimekuwa nijieleza moyoni peke yangu kama alivyosema Bwana Yesu kwamba wasamehe kwa kuwa hawajui walitendalo,” alisema Zuma huku akipigiwa makofi ya pongezi kutoka kwa makada wenzake hao wa ANC.
No comments