KWAMFANO UNAANZAJE KUKOSA KUFIKA TAIFA LEO
Soka mbinu, hicho ndicho kinachosubiliwa leo wakati makocha wa Yanga, Geogre Lwandamina na mwenzake wa Simba, Joseph Omog jinsi watakavyowatumia wachezaji wao kwa makini katika kuhakikisha wanaondoka na ushindi katika mchezo huo wa Ngao ya Jamii utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Moja ya sifa ya kocha ni jinsi anavyoweza kuwatumia wachezaji wake wa akiba kuingia kubadilisha mchezo na kuisaidia timu kupata ushindi.
Kama wewe ni shabiki basi ondoa shaka unapowaona wachezaji hawa wameanzia benchi kwani wanapoingia huenda wakabadilisha taswira ya mchezo pindi wakitokea benchi kwa timu zote mbili iwapo baadhi ya nyota watakaoanza kwenye kikosi cha kwanza watashindwa kufanya vyema.
Donald Ngoma
Anapewa nafasi kubwa ya kuanza katika mchezo wa kesho Jumatano dhidi ya Simba, lakini kutokana na hazina ya washambuliaji ambayo Yanga inayo, Ngoma anaweza kuanza kama mchezaji wa akiba.
Kutokana na uwezo wake mkubwa wa kusoma mabeki wa timu pinzani na kazi aliyonayo, ni wazi kuwa kama ataanzia benchi mechi ya Jumatano, anaweza kuwa tatizo kwa Simba.
Amissi Tambwe
Uwezo wake wa kuamua mechi akiingia kutokea benchi ulijidhihirisha msimu uliopita katika mechi ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya JKT Ruvu.
Katika mchezo huo, Tambwe aliingia na kuifungia Yanga mabao mawili huku mengine yakifungwa na Saimon Msuva na Obrey Chirwa.
Juma Abdul
Ni beki lakini ni mmoja wa wachezaji wanaoweza vyema kubadilisha mechi pindi wanapoingia kutokea benchi hasa pale timu inaposaka matokeo.
Msimu uliopita, beki huyo aliingia akitokea benchi kwenye mechi dhidi ya Toto Africans ambayo Yanga walikuwa wanahitaji ushindi ili wajiweke kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa.
Beki huyo sio tu aliiamsha Yanga bali ndiye aliyepiga krosi iliyozaa bao la ushindi kupitia kwa Amiss Tambwe.
Ibrahim Ajib
Uwezekano mkubwa uliopo ni Ajib kuanzishwa kwenye mechi hiyo lakini hata akiwekwa benchi, bado Simba hawatokuwa salama pindi akiingia.
Uwezo wake wa kupiga faulo, chenga na kumiliki mpira, inaweza chanzo kwa yeye kubadilisha mchezo iwapo atatokea benchi.
Msimu uliopita, Ajib alitokea benchi kwenye fainali ya Kombe dhidi ya FA na akawa chanzo kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbao FC kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Said Ndemla
Jina lake lilianza kujulikana pale alipotoa mchango mkubwa kwa Simba kutoka nyuma na kusawazisha mabao matatu dhidi ya Yanga katika mchezo wa mzunguko wa pili wa ligi kuu msimu wa 2013/2014.
Katika mchezo huo hadi mapumziko, Simba walikuwa nyuma kwa mabao 3-0 lakini kuingia kwa Ndemla na William Lucian kuliiamsha Simba ambayo ilisawazisha mabao hayo yote.
Mohammed Ibrahim
Kuna uwezekano mkubwa akaanzishwa kwenye kikosi cha kwanza dhidi ya Yanga lakini hata akitokea benchi, Ibrahim maarufu kama 'Cabaye' anamudu vilivyo kubadilisha mchezo.
Mchezaji huyo atakumbukwa kwa jinsi alivyobadilisha matokeo kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza msimu uliopita kati ya Yanga na Simba na hadi anaingia Simba walikuwa nyuma kwa bao 1-0 huku wakiwa pungufu lakini aliweza kuimarisha safu ya kiungo wakaweza kusawazisha bao hilo.
Shiza Kichuya
Mara kwa mara amekuwa akipata nafasi kwenye kikosi kinachoanza lakini kocha wa Simba, Joseph Omog alicheza kamali ya kutomwanzisha katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita dhidi ya Yanga.
Kichuya aliingia wakati Simba ipo nyuma kwa bao 1-0 huku ikiwa pungufu lakini alichangia kupatikana kwa bao la kusawazisha na kufunga la ushindi huku timu yake ikitoka kifua mbele kwa mabao 2-1.
Jonas Mkude
Siku hizi hana nafasi ya kudumu lakini ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kubadilisha upepo pindi anapoingia uwanjani akitokea benchi.
No comments