UKAWA NA OPERESHENII MPYA
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi waandamizi na wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), wameanzisha operesheni waliyoipa jina la Operesheni Ondoa Msaliti Buguruni (OBM).
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam viongozi wa kanda hiyo walisema wameamua kufanya hivyo baada ya kubaini ndani ya CUF kuna msaliti ambaye anakivuruga chama hicho huku akiwa na mpango wa kuvivuruga vyama vingine vya upinzani, hasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mbali na Chadema na CUF, vyama vingine vya siasa vinavyounda Ukawa ni NCCR-Mageuzi na NLD.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema wa kanda hiyo, Saed Kubenea, alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kikao walichofanya juzi kikiwajumuisha viongozi waandamizi wa CUF na baadhi ya wabunge wake.
Kubenea ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema operesheni hiyo haitakuwa ya vurugu bali itakuwa ya kidiplomasia.
“Tutaondoa msaliti mkuu na wale wa nyuma yake, kwa hiyo tumeamua kwa dhati kuwasaidia viongozi na wanachama wa CUF kwanza kumuondoa huyo msaliti mkuu na hao wengine watafuata kwa sababu ukitaka kufukuza ‘chizi’ wanasema mtupie na nguo zake, akiwa anakusumbuasumbua unachukua na nguo zake unatupa nje,” alisema Kubenea.
“Sisi kama Chadema Pwani tumeamua ‘serious’ kuwasaidia viongozi na wanachama wa CUF kumuondoa na kama pale Buguruni pana kitanda chake, mswaki au ndoo, sisi tutaviondoa na viongozi halali wa watarudi Buguruni.”
Pia, alisema wamebaini zipo njama zinazofanywa kwa kutumia mgogoro ndani ya CUF kuvuruga nguvu ya upinzani na Ukawa.
Alisema miongoni ya mikakati ya kufanikisha operesheni hiyo ni kufungua matawi yote ya CUF ambayo yalikuwa na nguvu, lakini yamekufa.
Alitaja matawi hayo ambayo alisema yalikuwa yamekufa kuwa ni pamoja na Chechinia, Ukanda wa Gaza, Cosovo na Palestina.
Kubenea alisema wameamua kufanya hivyo kwa sababu wamebaini mgogoro unaoendelea ndani ya CUF unadhoofisha Ukawa ili kufikia katika uchaguzi mkuu ujao uwe umesambaratika.
“Sisi janja hiyo tumeiona ya kuvuruga Ukawa 2020 na ndiyo maana tumeamua kuanzisha operesheni hii,” alisema Kubenea.
Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Riziki Shahari Mngwali, alisema msimamo wa wabunge wa Ukawa ni kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana katika shida na raha na kwamba tayari wabunge hao walishatoa msimamo wao wa kusaidia katika operesheni hiyo.
Mwenyekiti wa Chadema Ilala, Makongoro Mahanga, alisema wameamua kuingia katika operesheni hiyo ili kunusuru nguvu ya Ukawa na nguvu ya Chadema katika kanda hiyo.
“Sisi Kanda ya Pwani tunaathirika sana na mgogoro wa CUF kwa sababu makao makuu ya vyama hivyo yako katika kanda hii, kwa hiyo tumekaa na viongozi na baadhi ya wabunge wa CUF tumejiridhisha huu mgogoro umelenga kudhoofisha vyama vya upinzani na si vinginevyo,” alisema.
Aliongeza: “Tutakuwa bega kwa bega na wanaCUF katika kupambana na watu wanaotumika kusambaratisha chama.”
Tangu Agosti mwaka jana, CUF kimekuwa na mgogoro wa uongozi ambao mbali na mambo mengine umesababisha kufungwa kwa akaunti za fedha za chama hicho, hivyo kushindwa kutumia ruzuku inayotolewa na serikali kwa vyama vya siasa vyenye sifa.
No comments