Ads

SERIKALI NA BARICK KUKAA NA KUJADILI JUU YA MCHANGA WA MAKINIKA


HATIMAYE majadiliano kati ya Serikali na Barrick Gold Corporation ya Canada juu ya urejeshaji wa fedha ambazo nchi imepoteza kutokana na udanganyifu ambao umegundulika kwenye biashara ya makinikia ya kampuni yake ya Acacia yaatanza kesho.


Barrick ni mmiliki wa asilimia 63 ya hisa za Acacia Mining Ltd ambayo iligundulika ilikuwa ikifanya udanganyifu katika usafirishaji wa makinikia tangu migodi ya dhahabu ya kampuni hiyo ianze kusafirisha mwaka 1998.

Mwezi uliopita, Mwenyekiti wa Barrick, Prof. John Thornton alifanya mazungumzo na Rais John Magufuli na kukubali kulipa fedha ambazo zitakuwa zilipotea. Haikutajwa tarehe ya kuanza kwa mazungumzo hayo, hata hivyo.

Lakini akizungumza katika sherehe ya makabidhiano ya nyumba 50 za watumishi wa afya kwa mikoa ya Geita, Simiyu na Kagera zilizojengwa na Taasisi ya Mkapa Foundation kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto jana, Rais Magufuli alisema mazungumzo hayo yataanza kesho.

Ripoti iliyowasilishwa mwezi uliopita na Prof. Nehemia Osoro ilisema nchi inaweza kuwa imepoteza mpaka Sh. trilioni 489 katika kodi na mali (madini) kwa miaka 19 iliyopita kwenye biashara hiyo ya madini inayofanywa na Acacia.

Kati ya fedha hizo, kiwango cha kodi kilitajwa kuwa Sh. trilioni 108.

Prof. Osoro ni mwenyekiti wa kamati maalum iliyochunguza masuala ya sheria na kiuchumi kuhusiana na mchanga wa madini unaosafirisha nje ya nchi.

Kufuatia ripoti hiyo ambayo pia ilionyesha Acacia haina usajili hivyo uhalali wa kuchimba madini nchini, Rais John Magufuli alizuia usafirishaji wa makinikia kwenda nje ya nchi na kudai marejesho ya fedha hizo.

"Kesho kutwa (Jumatano) mazungumzo yanaanza na wale waliokuwa wanatuibia ibia," alisema Rais Magufuli katika hotuba yake ya shukrani kwa ajili ya mradi huo.

"Na nilishamwagiza (Naibu) Waziri wa Nishati na Madini hakuna kutoa leseni mpya katika uchimbaji wa madini hadi tujipange upya, akitoa na yeye amekwenda," alisema Rais Magufuli.

Alisema kinachotakiwa katika uchimbaji wa madini ni faida kwa watu wote, "wageni wachimbe na sisi watuachie faida".

Alisema uchimbaji wa madini unaoacha mashimo yanayohatarisha kutokea kwa tetemeko la ardhi bila faida kwa wazawa hautakiwi.

Kabla ya kamati ya Prof. Osoro kugundua kuwa Acacia ilikuwa ikikwepa kodi na kufanya udanganyifu wa kiwango cha biashara, Mei 24, mwaka huu kamati ya kwanza iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma iligundua kiwango cha madini katika makontena 277 ya kampuni hiyo ni kikubwa kuliko taarifa rasmi.

UPATANISHI
Acacia, hata hivyo, ilitangaza kufungua 'kesi' ya kuomba upatanishi wa mgogoro huo Jumanne iliyopita.

Taarifa iliyotolewa na Acacia ilisema kampuni hiyo imewasilisha taarifa hiyo ya kutafuta upatanishi kwa niaba ya kampuni zake tanzu za Bulyanhulu Gold Mine (BGML) na Pangea Minerals Limited (PML) inayomiliki mgodi wa Buzwagi.

Kampuni hiyo ya Uingereza inamiliki pia mgodi wa dhahabu wa North Mara, lakini ni miwili hiyo ambayo mali yake huhusisha uchenjuaji wa makinikia.

Migogoro ya kimataifa ya kiuwekezaji hutatuliwa na ama Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) au Chemba ya Kimataifa ya Biashara (ICC).

Ingawa taarifa ya Acacia haikueleza imefungua wapi ombi lake la kutaka upatanishi wa mgogoro wa makanikia, chanzo cha kuamianika kiliiambia pande hizo mbili zitaketishwa pamoja ICSID yenye makao yake makuu Washington DC, Marekani.

"Taarifa za kusudio hili zinahusu mgogoro wa sasa kati ya Serikali ya Tanzania na kila moja kati ya BGML na PML kusuluhishwa," ilisema Acacia katika taarifa yake iliyowekwa kwenye mtandao wake wa kompyuta na kueleza zaidi:

"Hii ni kuendana na mchakato wa utatuzi wa migogoro uliokubaliwa na Serikali ya Tanzania katika Makubaliano ya Uendelezaji Madini na BGML and PML.

"Uwasilishaji wa taarifa ya kutafuta upatanishi hii kwa wakati huu ni muhimu kwa ajili ya kuilinda kampuni, lakini, pamoja na hatua hii, Acacia bado ina mtazamo kuwa mazunguzo nje ya vyombo rasmi ndiyo njia bora ya utatuzi wa migogoro iliyopo na kampuni itaendelea kufanya jitihada kufanikisha hili."

Acacia ilisema serikali pia imeiarifu Barrick, kampuni yake mama, kuwa kwa sasa ingependa kuendelea na mazungumzo yao, na hivyo "Acacia haitoshiriki moja kwa moja kwenye mazungumzo hayo wakati yatakapoanza."

"Suluhisho lolote litakaloweza kubainishwa kutokana na mazungumzo hayo litalazimika kupitishwa na Acacia, na kampuni itashirikiana na Barrick kwa hali na mali kusapoti mazungumzo hayo."

No comments

Theme images by andynwt. Powered by Blogger.