MWITIKIO WA KANUNI ZA LIGI KUU BADO HAKIJAELEWEKA...
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema bado mwitikio ni mdogo kwa wadau wa soka kuwasilisha maoni na mapendekezo mbalimbali kuhusu marekebisho ya kanuni za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza.
TFF ilitangaza klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu Bara na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao kwamba kipindi hiki ni cha kuwasilisha maoni na mapendekezo mbalimbali kuhusu marekebisho ya kanuni za ligi husika.
Afisa habara wa TFF, Alfred Lucas alisema licha ya kutangaza klabu kuwasilisha mapendekezo mbalimbali kuhusu marekebisho ya kanuni za ligi bado mwitikio umekuwa mdogo jambo linalowashangaza.
Alisema hawataki baadae watu waje kulalamika pindi wanapobanwa na kanuni hizo wakati walikuwa na muda wa kupendekezwa kurekebishwa kwa kanuni mbalimbali za uendeshaji wa ligi.
Alfred aliwataka wadau wa klabu hizo kujitokeza kuwasilisha maoni hayo ili yafanyiwe kazi na kupunguza malalamiko mbalimbali katika ligi msimu ujao.
"Tumetangaza wadau na wanafamilia wa mpira wa miguu Tanzania kuwasilisha mapendekezo kuhusu marekebisho ya kanuni za ligi kupitia anwani au barua pepe ya bodi la Ligi au walete moja kwa moja TFF, lakini ni wachache sana wamejitokeza.
"Tumefanya hivi mapema ili watu watoe madukuduku yao kuhusu kanuni za ligi ili kurekebisha kabla ya ligi msimu ujao haijaanza kwani wanavyoendelea kukaa kimya maana yake kanuni zitabaki vile vile na tutakapozitumia kwa makosa yatakayofanywa basi wasianze kulalamika"alisema Lucas
Alisema maoni hayo yakiwasilishwa yatafanyiwa kazi na Bodi ya Ligi kabla ya kupelekwa kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji.
No comments