HAYA HAPA MAJINA SITA MAPYA JAGWANI...
IBRAHIMU Ajibu tayari ni mali ya Yanga na amepewa jezi namba 10 ambayo ilikuwa ikivaliwa na Matheo Anthony ambaye maji yamezidi unga.
Sasa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Yanga, Hussein Nyika, amewasisitiza mashabiki wa klabu hiyo kwamba watulie kuna mambo mazuri yanakuja kwani usajili wa Ajibu ni mwanzo tu.
Kiongozi huyo ametamka kwamba katika listi ambayo Kocha George Lwandamina amewaonyesha mpaka dakika hii, kuna viungo sita wa maana wa ndani na nje ya nchi ambao wanahitaji kuwafanyia mchujo.
Ameongeza kwamba wamepanga kutumia nguvu kubwa kwenye safu ya kiungo ambayo imekuwa ikiwapa shida kwa muda mrefu na wamepania kuhakikisha kuwa timu watakayoisuka itaendana na ushindani wa msimu ujao.
Alisema kwamba wameona hali halisi inayoendelea kwenye usajili wa klabu mbalimbali za Ligi Kuu Bara, lakini wao wamepania kusuka Yanga ambayo iotashiriki pia Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tunaendelea na usajili kikubwa tunacholenga sasa na kiukweli tunataka kufanya mapinduzi makubwa ni katika safu ya kiungo ambayo kwa muda mrefu tumekuwa ikitusumbua kwa namna moja ama nyingine,” alisema Nyika.
“Tulichofanya kama kamati tumekubaliana kocha ndiye aamue ni mchezaji gani anamtaka, tumefanikiwa kumsafirisha ili akafuatilie viwango mbalimbali vya wachezaji tunaowataka na mpaka sasa ana majina sita ya viungo tofauti katika meza yake.
“Majina hayo atayaamua yeye ni wachezaji gani anaona ni mwafaka kwetu ili sisi uongozi tumalizane nao baada ya kupata baraka zote kutoka kwake, tunataka kuona kama tunamsajili kiungo mkabaji awe mtu wa kazi kweli lakini kama tukisajili kiungo mchezeshaji awe ni mtu anayejua sawasawa,” alisisitiza lakini hakuweka wazi ni wachezaji gani kwa madai kwamba atakuwa anauza silaha.
“Katika hayo majina sita mapya tunataka watu wanne wa uhakika ambao, anayecheza kiraka atakuwa na nafasi kubwa ya kusajiliwa.”
Tayari Mwanaspoti linafahamu kwamba Yanga katika mawindo hayo ina viungo Cleatus Chota Chama (Zambia), Fernando Bongnyang (Pichani) (Cameroon) ambaye tayari yupo Dar es Salaam, Kabamba Tshishimbi (DR Congo) na mmoja kutoka Msumbiji.
Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, aliongeza kuwa wanasajili kutokana na mapungufu waliyoyaona katika kikosi na si kufuatilia wapinzani wao wamesajili wachezaji wa aina gani ili kuweza kushindana nao.
“Licha ya kufunga mabao mengi msimu uliopita kuliko timu yoyote, tumeona kuwa safu yetu ya ushambuliaji pia bado ina mapungufu kwa hiyo ni vizuri kuiboresha zaidi hasa tukizingatia tuna mashindano makubwa ya kimataifa,” alisema Mkwasa.
MSEMAJI MBEYA CITY
Habari ambazo Mwanaspoti ilizipata jana mchana ndani ya uongozi wa Yanga ni kwamba klabu hiyo ilikuwa kwenye mazungumzo na Msemaji aliyemaliza mkataba wake na Mbeya City, Dismass Ten.
Habari zinasema kwamba Yanga inataka Dismass achukue kitengo hicho ambacho kimekuwa wazi kwa muda sasa baada ya kuachana na Jerry Muro aliyekuwa amefungiwa na TFF.
KASEKE HUYO SINGIDA
Kiungo anayemaliza mkataba na Yanga, Deus Kaseke, huenda akasaini mkataba na Singida United muda wowote kuanzia sasa baada ya mazungumzo yao kwenda vizuri na kufikia hatua za mwishoni.
Kaseke ambaye ameitumikia Yanga kwa miaka miwili, hajaongeza mkataba na amekuwa akihusishwa na timu hiyo ya Singida ambayo inanolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Hans Van Pluijm.
Singida United inaendelea na usajili wake wa mwisho mwisho na tayari timu hiyo imeingia kambini huku ikiwa imesajili baadhi ya nyota wazawa ambao ni Miraji Adam, Kenny Ally, Atupele Green na Pastory Athanas.
Nyota wa kigeni waliosajiliwa na Singida United ni Elisha Muroiwa, Wisdom Mtasa, Tafadwaza Kutinyu, Simbarashe Nhivi, Shafik Batambuze, Danny Usengimana na Michael Rusheshangoga ambaye yuko mbioni kusaini mkataba.
Mkurugenzi wa Masoko wa klabu hiyo, Festo Richard, alikiri kuwepo kwa mazungumzo kati yao na Kaseke.
“Kila kitu kinakwenda vizuri ingawa kilichokwamisha hadi sasa ni suala la pesa ya usajili, anahitaji pesa nyingi. Mazungumzo yanaendelea na tunaamini tutafikia makubaliano na muda wowote atasaini,” alisema.
Wakati huo huo, Festo alisema kuwa nyota wao wawili wa kigeni wanatarajia kujiunga na kambi yao wiki ijayo Jumatatu.
Aliwataja nyota hao kuwa ni Usengimana pamoja na Rusheshangoga.
No comments