JESHI LA NIGER LAUWA RAIA KIMAKOSA...
Jeshi la Niger limewaua kimakosa raia 14 waliodhaniwa kuwa wapiganaji wa Boko Haram katika eneo la mashambani la Kusini mashariki kulingana na maafisa.
Waathiriwa wote wakiwa wakulima wasio na silaha zozote walikuwa katika eneo lililotengwa katika kijiji cha Abadam karibu na mpaka na Nigeria.
Watu wawili walikuwa kutoka Niger huku wengine wakitoka Nigeria.
Maelezo kuhusu operesheni hiyo na kwa nini watu hao walikuwa katika eneo hilo hayajabainika.
Wapiganaji wa Boko Haram wamekuwa na makao yao nchini Nigeria lakini wamekuwa wakihusishwa na mashambulizi ya kuvuka mpaka.
Maelfu ya watu wamewachwa bila makao katika eneo la Kusini mashariki la jimbo la Diffa na raia kupigwa marufuku kuzuru maeneo tofauti.
Hatahivyo wengi wamekuwa wakirudi ili kuangalia mimea yao kulingana na waandishi.
Kulikuwa na ripoti kinzani kuhusu opepersheni hiyo ya jeshi.
Kituo cha habari cha AFP kilisema kuwa shambulio la angani liliua kundi hilo lilipokuwa likirudi kuangalia mimea yao.
Lakini chombo cha habari cha Reuters kilisema kuwa wanajeshi walikuwa wakipiga doria katika eneo hilo wakati walipofanya shambulio.
Yahaya Godi katibu mkuu wa eneo la Diffa alisema kuwa Abadam ni kijiji kilichopo katika eneo hatari na limetengwa kwa muda mrefu ..na kwamba mtu yeyote anayepatikana katika eneo hilo hutambulika kuwa mwanachama wa Boko Haram.
Jimbo la Diffa limekumbwa na misururu ya mashambulizi yanayotekelezwa na Boko Haram katika miaka ya hivi karibuni.
Siku tatu zilizopita, washukiwa wa kundi hilo waliwaua watu tisa na kuwateka wengine kadhaa wakiwemo watoto.
No comments