Ads

MGHWRA AANZA NA MOSHI


Image result for advertise here





Image result for mghwira

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, amewaonya wakurugenzi wa halmashauri sita za wilaya mkoani humo kuacha tabia za kizamani za kuwabania taarifa madiwani wao na kuwapa vitini vyenye taarifa mbalimbali za umma siku moja kabla ya kikao,badala yake ameagiza wapelekewe siku 14 kabla ya baraza kufanyika.


Aliagiza hayo wakati akizungumza kwa mara ya kwanza na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.

“Wapeni taarifa siku 14 kabla ya kikao cha Baraza la Madiwani ili waweze kupitia na kujua kilichoandikwa, hiyo dhana mliyonayo ya kuwapa madiwani vitini vyenye taarifa siku moja au mbili kabla ya kikao haina tija,” alisema.   

Aidha, aliwaonya watumishi wa umma kutojiingiza katika biashara ya kuvusha chakula kwa njia ya magendo kwenda nchi jirani, huku pia akitumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Wilaya za Siha, Hai, Moshi, Rombo, Mwanga na Same, kutouza mazao ya chakula yakiwa shambani kabla ya kuvunwa.

Wakulima katika baadhi ya maeneo nchini, wana desturi mbaya ya kuuza chakula kikiwa shambani hasa mahindi na maharage kwa bei ya kutupa, bia kujua kwamba kufanya hivyo kunawadidimiza kiuchumi na kuendelea kuwa masikini.

Aidha, hali hiyo imekuwa ikisababisha baadhi ya kaya kukumbwa na upungufu wa chakula na hivyo kuathiri utaratibu wa kawaida wa kutokuwa na uhakika wa kula milo mitatu kwa siku.

Awali, Katibu Tawala Msaidizi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Kilimanjaro, anayeshughulikia Serikali za Mitaa, Jasper Ijiko, akitoa ufafanuzi kuhusu mkakati huo wa Anna Mghwira, alisema kila halmashauri inapaswa kuhakikisha inawasisitiza wananchi kuweka akiba ya chakula.

“Mkuu wa mkoa amepewa mamlaka ya kikatiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 61 (1) na (4) pamoja na Sheria ya Tawala za Mikoa, Sura ya 97, Kifungu cha 5 (3) kusimamia shughuli zote za serikali, kuzisimamia na kuzilea halmashauri za wilaya," alisisitiza.

No comments

Theme images by andynwt. Powered by Blogger.