Ads

SUMAYE ADAI CCM WANAHUSIKA KUJIUZULU KWA MADIWANI



Image result for sumaye

MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye, amedai kunusa hujuma kwa madiwani wa chama hicho mkoani Arusha ambao baadhi yao walihamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivi karibuni na kuibua gumzo.


Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka kumi mfululizo (1995-2005) wakati wa serikali ya awamu ya tatu, alisema anaamini kuwa madiwani waliohamia CCM hawakufanya hivyo kwa hiari yao bali walishinikizwa na viongozi wa chama tawala.

Sumaye aliyasema hayo jana alipozungumzia masuala mbalimbali na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kwenye ofisi ya Chadema Kanda ya Pwani, iliyoko Magomeni.

Hivi karibuni, madiwani watano wa Chadema mkoani Arusha waliripotiwa kuhama chama hicho na kuhamia CCM.

Jiji la Arusha linaongozwa na Chadema ambayo ndiyo yenye madiwani wengi baada ya kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu uliopita dhidi ya CCM, huku pia Godbless Lema akitetea kiti cha ubunge wa jimbo hilo la Arusha Mjini.

Akieleza zaidi, Sumaye alisema wanachama wa chama chochote wana haki ya kuhamia chama chochote cha siasa, lakini walichofanya madiwani wa Chadema mkoani Arusha ni kutii shinikizo kutoka kwa viongozi wa CCM.

“Haiwezekani wahame wote kwa wakati mmoja na cha ajabu, kila diwani ameandika barua inayofanana na ya mwenzake… sasa hii inaonyesha kuwa hawahami kwa mapenzi yao bali kwa kushinikizwa,” alisema Sumaye.

Aidha, Sumaye alidai kuwa hivi sasa, hakuna demokrasia nchini kwa sababu chama tawala hakikubali kuondoka madarakani na kitalinda nafasi yake hiyo kwa kuvinyima pumzi vyama vya upinzani, ikiwamo njia hiyo ya kuwalaghai baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani na pia njia ya kutumia vyombo vya dola kuwanyanyasa.

Alizungumzia pia uhuru wa habari, akisema kuwa nao umeathirika kwa kiasi kikubwa kwa sababu hakuna uhuru wa kutosha wa kutoa habari, kupokea habari, kutoa maoni na kufanya mawasiliano bila kuingiliwa na chombo chochote.

Alisema kwa misingi ya demokrasia, mtu yeyote ana haki ya kutofautiana mawazo na kiongozi na kufanya hivyo siyo kosa.

No comments

Theme images by andynwt. Powered by Blogger.