KILICHOMPONZA Boss wa Tanesco Kutumbuliwa Hichi Hapa..........
HATUA ya Shirika la Umeme ya kupandisha bei ya umeme bila kushirikisha mamlaka nyingine za Serikali, zimemgharimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Felchesmi Mramba, ambaye jana amefutwa kazi na Rais John Magufuli.
Kabla ya kutengua uteuzi wa Mramba, Rais Magufuli ambaye jana alisali mjini Bukoba katika kanisa la Bikira Maria, Mama mwenye Huruma la mjini Bukoba, alisema Tanesco haikumshirikisha yeye, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Ewura juzi ilitangaza kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 baada ya Tanesco kuomba gharama zipande kwa asilimia 18.19, lakini hatua hiyo ilisitishwa na Profesa Muhongo. “Waliopandisha umeme hawakuja kuniuliza hata mimi kiongozi wa nchi, hawakuuliza hata waziri mwenye dhamana, ya nishati hawakumuuliza hata Makamu wa Rais, Waziri Mkuu haiwezekani mtu akae pekee yake na afanye maamuzi yake pekee bila kushirikisha mamlaka nyingine,” alisema Rais.
Ateua bosi mpya
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU, Gerson Msigwa ilieleza kuwa Rais Magufuli baada ya kutengua uteuzi wa Mramba, amemteua Dk Tito Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco.
Mwinuka ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) na hadi uteuzi wa jana, alikuwa ni Mkuu wa Idara ya Mekanika na Uhandisi wa Viwanda Chuo cha Uhandisi na Teknolojia (CoET) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. #HabariLeo
No comments