Ads

Haya sasa Tshishimbi kaamua kutengeneza ukuta wa yanga



Image result for tshishimbi yanga


KIUNGO ambaye ni habari ya mjini kwa mashabiki wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi, ameangalia ukuta wa timu hiyo akawaambia viongozi anawaletea bonge la beki fundi.
Tshishimbi ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo aliyenunuliwa na Yanga akitokea Mbabane Swallows ya Swaziland, amewahakikishia mabosi hao kuwa kama beki huyo akitua na kushirikiana vizuri na waliopo, hao mastraika wanaoogopwa akina Emmanuel Okwi hawatafua dafu.
Habari za ndani ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba mchezaji huyo alifikia hatua hiyo baada ya kuona aina ya uchezaji wa timu za Simba na Lipuli walizovaana nazo.
Yanga inahaha kusaka beki wa kati wa kuziba nafasi ya Mtogo Vincent Bossou aliyemaliza mkataba, baada ya kushindwa kufanya usajili mpya dakika za mwishoni kutokana na kubanwa na kanuni za Ligi Kuu Bara.
Taarifa kutoka ndani ya mabosi wa Yanga ni kwamba Tshishimbi amewakabidhi jina la beki anayemuamini ataweza kutuliza ukuta wao ambao kwa sasa upo chini ya Andrew Vincent ‘Dante, Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Mwanaspoti limejiridhisha kwamba viongozi hao wamepewa jina la beki huyo na muda wowote wataanzisha mazungumzo naye kwa ajili ya usajili wa dirisha dogo linalofunguliwa Novemba hadi Desemba.
“Tuliamua kumuuliza Tshishimbi kama anaweza kumjua mchezaji yeyote anayeweza kutufanyia kazi katika safu yetu ya ulinzi hasa beki wa kati,” alisema bosi mmoja wa Yanga.
“Na yeye ametuambia anamjua beki mmoja rafiki yake ambaye hana wasiwasi atakuja kufanya kazi nzuri hapa na jina lake ameshatupatia, tumeshampa kocha kwa ajili ya yeye naye kuona namna ya kumfuatilia. Ila kwa sasa hatuwezi kulitaja jina hilo, bado ni suala la ndani. Tutajiridhisha kwanza kabla ya hatua zaidi.”
Lakini Mwanaspoti lilimuuliza Tshishimbi kuhusiana na hilo naye akasema: “Ni kweli nimefanya maongezi na viongozi juu ya huyo beki, ni rafiki yangu ingawa sikuwa nacheza naye timu moja. Lakini kwa jinsi nilivyowaona washambuliaji wa hapa, jamaa akija atawadhibiti sana na ameniambia yupo tayari kuja kama Yanga watamfuata.”
Mechi ijayo ya Yanga ni ya ugenini dhidi ya Njombe Mji itakayochezwa Septemba 6. Njombe alipigwa mabao 2-1 na Prisons mechi ya kwanza huku Yanga ikitoa sare ya 1-1 na Lipuli.

No comments

Theme images by andynwt. Powered by Blogger.