Baada ya Simba kumtibu mwanaye aamua kuihama Yanga
Baba mzazi wa mtoto Mwamvita Abdulilah aliyepewa msaada wa matibabu wa Sh 2milioni na klabu ya Simba katika Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ameamua kuhama kuishabikia Yanga na kujiunga miamba hiyo ya Msimbazi.
Mwamvita aliyelazwa hospitalini hapo kwa zaidi ya miezi miwili akisubiri upasuaji, alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kushindwa kupumua vizuri kutokana na kuwa na tundu kwenye moyo amepona na anatarajia kuruhusiwa muda wowote kuanzia sasa.
Baba mzazi wa mtoto huyo, Abdulilah Bakari alisema amehangaika na mtoto huyo kwa takribani miaka mitatu na hivi sasa nashukuru Mungu kwani amepona baada ya kupatiwa matibabu.
"Nashukuru sana kwa dhati Simba, mimi nilikuwa Yanga damu damu, lakini kutokana na kile ambacho Simba wamenifanyia kutoa Sh2 milioni kumtibia mwanangu nimehama rasmi na sasa nimehamia Simba mimi na familia yangu," alisema Abdulilah.
Naye mtoto Mwamvita alisema anashukuru wanasimba wote kwa kujitoa kuokoa maisha yake, "sasa nitaweza kurudi masomoni nashukuru kwa nafasi hii waliyonipa naomba Mungu awaongezee walipopunguza."
Akizungumza MCL Digital leo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi alisema baada ya kupatiwa fedha hizo za matibabu, walimfanyia upasuaji Mwamvita Agosti 24 mwaka huu.
Alisema upasuaji huo ulifuatia baada ya viongozi na wachezaji wa Simba kutembelea taasisi hiyo Agosti 7 mwaka huu katika maadhimisho ya Simba Day na kukutana na Mwamvita ambaye alikuwa akisubiri kufanyiwa upasuaji.
"Walikuja kutoa msaada kwa watoto wenye matatizo ya moyo na ndipo walipokutana na Mwamvita na kutoa msaada huo, tunashkuru sana kwa msaada huu na tunakaribisha klabu nyingine kutoa msaada pamoja na TFF ili watoto wengi zaidi wasaidiwe," alisema.
Alielezea kuhusu afya ya Mwamvita, Profesa Janabi alisema kwa sasa anaendelea vizuri na ameshapona tatizo linalomsumbua baada ya kufanyiwa upasuaji.
"Tulimfanyia upasuaji mkubwa wa kufungua kifua, amepona na tunatarajia kumruhusu kurudi nyumbani wakati wowote kuanzia sasa," alisema.
No comments