SIMBA,YANGA na SINGIDA UNITED WAITISHA NJOMBE MJI....
Dar es Salaam. Usajili unaofanywa na Simba, Yanga na Singida United umeonekana kumpa hofu kocha msadizi wa Njombe Mji, Mrage Kabange.
Njombe Mji ya Njombe imepata nafasi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao kwa mara ya kwanza ikipanda daraja pamoja na Singida United ya Singida na Lipuli ya Iringa.
Mrage alisema jinsi klabu zinavyofanya usajili wa maana inaonyesha kuwa ligi ya msimu ujao itakuwa kiboko, lakini wao watapambana hivyo hivyo mpaka kitaeleweka.
"Safari hii naona timu zimeamua angalia kama Simba wameonekana kabisa wamepania na wamechoka na manyanyaso ya miaka minne waliyopata kutoka kwa watani zao Yanga.
"Singida nayo imepanda daraja, lakini imeonekana ina nguvu ya fedha na inasajili yoyote hivyo ligi ya msimu ujao usipojipanga umeumia,"alisema Mrage.
Mrage alisema wanatamani kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi, lakini fedha ndio kikwazo kwao hivyo anaamini wachezaji chipukizi waliowasajili wataibeba timu hiyo kwenye ligi.
"Sisi hatuna fedha ya kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi au wachezaji wenye majina makubwa, lakini hawa hawa chipukizi tunaowasajili wanaweza kufanya maajabu kwenye ligi. Tutapambana tu mpaka kitaeleweka," alisema Mrage.
No comments