MWAPACHU AAMUA KUSTAAFU NA KUJIFUTA KABISA
Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kada wa chama cha mapinduzi (CCM), Balozi Mwapachu jana tarehe 13/07/2017 ameamua kustaafu na kutoka kabisa katika Bodi ya Wakurugenzi ya kampuni inayojihusisha na uchimbaji wa madini Acacia
Acacia wamethibitisha Balozi Mwapachu kustaafu kwake na kujiondoa katika Bodi ya Wakurugenzi lakini pia wamemshukuru Balozi Mwapachu kwa muda wake wote wa miaka mitatu ambao walikuwa naye katika bodi hiyo kwani alikuwa na mchango mkubwa.
"Tunamtakia maisha marefu , bodi ya wakurugenzi, wakurugenzi na timu ya usimamizi tunakubaliana na Balozi Mwapachu kwa maamuzi yake, ila tunashukuru kwa msaada wake kwa kampuni kwa kipindi chote tulichokuwa naye" alisema taarifa ya Acacia
Kutokana na mabadiliko hayo Acacia wamefanya mabadiliko ya Bodi ya Wakurugenzi na sasa bodi ya ACACIA itajumlisha wanachama saba ambao watakuja kubainishwa siku za usoni.
Siku za karibuni kampuni ya ACACIA ilidaiwa kuwepo Tanzania bila usajili wowote, na kudaiwa kufanya biashara ya madini kinyume na utaratibu na sheria za nchi kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na tume mbili zilizoundwa na Rais John Pombe Magufuli kuchunguza madini mbalimbali ambayo yapo kwenye mchanga wa madini unaofahamika kama makinikia.
No comments