MMH YANGA WAPATA JEMBE LINGINE
MABOSI wa Yanga, wajanja sana, baada ya kufahamu wazi kuwa msimu ujao hawatakuwa na winga wao teleza, Simon Msuva, anayejiandaa kwenda kucheza soka la kulipwa Morocco, fasta wameamua kufanya jambo moja la maana.
Ili kuhakikisha kasi ya kikosi chao inakuwa katika mwendo ule ule, wamemnasa kiberenge kipya ili kumrithi Msuva katika kuwalisha mipira akina Ibrahim Ajibu, Donald Ngoma na washambuliaji wengine wa timu hiyo ya Jangwani.
Winga teleza huyo mpya aliyenaswa na mabosi hao wa Yanga ni Issa Yahya ‘Akilimali’ ambaye walimdaka juu kwa juu na kuamua kumficha katika moja ya maeneo tulivu ya Jiji la Dar es Salaam ili kumpa mkataba wa kuitumikia timu hiyo.
Kiberenge hicho kimetajwa kuwa na sifa za kukimbia kwa kasi, kupiga krosi zenye macho sambamba na kufumua mashuti kulenga lango, kama alivyo Msuva aliyekuwa Mfungaji Bora msimu uliopita akilingana na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting kila mmoja akitupia kambani mara 14.
Kabla ya kudakwa na mabosi wa Yanga, winga huyo alikuwa kwenye mipango ya kujiunga na Lipuli Iringa, lakini wanene wa Jangwani waliposikia sifa zake, wakaacha kila kitu ili kumweka sawa kabla ya kuingia naye sehemu tulivu na kumpiga lanchi na kinywaji na kumuuliza: “Kwani shida yako nini? Si unataka kucheza soka na kupanda ndege, basi we tulia.”
Kwani dogo huyo alikuwa na la kusema, alitulia kimya akisikilizia mabosi hao.
Licha ya kwamba mabosi wa Yanga wamekuwa wasiri, lakini Mwanaspoti linafahamu kuwa Yahya alionwa na Lipuli kwenye michuano ya Ndondo Cup akitokea masomoni Uganda na alikuwa miongoni mwa wachezaji 10 waliopendekezwa kusajiliwa na timu hiyo iliyorejea Ligi Kuu msimu huu.
Winga huyo jana Jumatatu asubuhi alifanya mazoezi na Lipuli kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam lakini baada ya mazoezi hayo alikutana na simu ya viongozi wa Yanga ambao walimweka kati ili kumsainisha.
Kutokana na umuhimu wa usajili wa kiberenge huyo, kocha George Lwandamina aliamua kufuta mazoezi ya jana jioni kwa madai kwamba wachezaji wamechoka ili kutoa fursa kwa viongozi wake kumalizana na winga huyo ili kuziba nafasi ya Msuva anayeenda Morocco kucheza soka la kulipwa.
Habari kutoka ndani ya Kamati ya Usajili ya Yanga zilisema kwamba kutokana na hofu ya kumpoteza nyota huyo ambaye amerejea nchini kutoka Uganda alikokwenda kusoma, waliamua kuzungumza naye ili kumalizana naye kabla ya kumruhusu ahudhurie mazoezi ya timu hiyo leo Jumanne.
YAMVUTA BEKI WA RAYON
Wakati mabosi wa Yanga wakiwa mbioni kumalizana na winga huyo, kocha Lwandamina aliwapa jina la beki Mnyarwanda, Thierry Manzi ili ajiunge na klabu hiyo, iwapo Mnigeria Henry Okoh atashindwa kufanya vizuri majaribio yake.
Beki huyo wa kati anacheza Rayon Sports ya Rwanda na Jumamosi iliyopita alikuwa na timu ya Taifa ya nchi hiyo, Amavubi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, alikocheza kwa kiwango cha juu na kumzuia straika wa Stars, John Bocco asiweze kuleta madhara langoni mwao na mechi kuisha kwa sare ya 1-1.
Mmoja wa vigogo wa Yanga aliliambia Mwanaspoti kwamba Lwandamina amevutiwa na uwezo wa beki huyo na kusema kwamba anakidhi mahitaji yake hivyo viongozi hao wajiandae kusafiri kwenda Kigali kama Okoh atachemka.
Yanga mpaka sasa inapambana kuimarisha beki yake ya kati na kiungo mkabaji baada ya kujiridhisha na eneo la ushambuliaji ambalo limeongezwa Ibrahim Ajibu atakayecheza na wakali, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Obrey Chirwa.
Katika mipango yao yupo Erasto Nyoni ambaye wanataka kumsajili kutoka Azam pamoja na kiungo wa Mbeya City, Raphael Daudi, ambaye tayari wamezungumza naye na kukubaliana kila kitu.
Mambo yakienda vizuri mabingwa hao wa Bara wanaweza kuwa moto zaidi.
No comments