JUUKO MURSHID AZIWEKA SIMBA NA YANGA ROHO JUU
KIKOSI cha Simba tayari kimeanza mazoezi yake ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuanza Agosti, mwaka huu.
Hata hivyo, timu hiyo kuna uwezekano mkubwa msimu ujao isiwe na beki wake wa kati, Mganda Juuko Murshid ambaye kuna taarifa kuwa amegoma kurudi nchini akitokea Uganda kwa ajili ya kuendelea na majukumu yake klabuni hapo.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo Champion Ijumaa limezipata zimedai kuwa kuna timu nyingine ambayo imekuwa ikitajwa kumuwania na ndiyo maana uwezekano wa yeye kuendelea kubaki Simba kuwa shakani.
Simba imekuwa ikiingia katika mvutano wa mara kwa mara juu ya mchezaji huyo ambapo awali ilielezwa kuwa wanataka kumuacha kutokana na nidhamu yake kuwa tata huku mwenyewe akitaka kuondoka kwa kuwa amekuwa akiingia katika mgogoro na viongozi mara kwa mara. Upande wa pili Yanga wanatajwa kumuwania kwa nguvu.
Akizungumza na gazeti hili, kigogo mmoja wa Simba, alitamka: “Hata hivyo taarifa tulizonazo ni kwamba, kuna mtu tayariYanga wameshamtuma nchini Uganda kwa ajili ya kuweka mambo sawa kwa sababu hivi sasa wana fedha za usajili.
“Lakini ninachoweza kusema ni kwamba, wasitegemee kuwa watampata kirahisi kwa sababu bado ana mkataba na sisi mpaka Desemba, mwaka huu.
“Kwa hiyo hatuwezi kumuachia akajiunge na Yanga, yani ni bora tumtoe kwa mkopo katika timu yoyote ya nje ya nchi mpaka hapo mkataba wake utakapomalizika,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Alipotafutwa Juuko kwa njia ya simu ili aweze kuzungumzia suala hilo hakupatikana, lakini alipoulizwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe kuhusiana na hilo alisema kuwa hana cha kusema.
Kwa upande wao Yanga kupitia kwa katibu mkuu wa klabu hiyo, Charles Mkwasa, alipoulizwa alisema: “Taarifa hizo bado hazijafika mezani kwangu hivyo siwezi kuzizungumzia ila Juuko ni mchezaji mzuri ambaye timu yoyote ilie hapa nchini ingependa kuwa naye.”
No comments