SUMAYE KAAMUA KUVUNJA UKIMYA
Waziri Mkuu Mstaafu na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Mh. Fredrick Sumaye amewataka viongozi waliopo madarakani kutotumia visasi kwa viongozi waliohamia upinzani kwani visasi hupelekea viongozi kuwa wezi.
Akizungumza jana na wanahabari jijini Dar es salaam Mh. Sumaye amesema kwamba viongozi waliowahi kuwa katika chama tawala kisha kuhamia upinzani wamekuwa katika wakati mgumu kwa kusakamwa na kunyang'anywa mali ambazo awali walikuwa wakimiliki kihalali ikiwa ni pamojan na kuongelewa maneno mabaya.
"Tukianza kujenga visasi vya kisiasa hakuna atakayepona na niwahakikishie atakayepona ni yule ambaye atahama nchi baada ya uongozi wake kufikia ukomo. Visasi vinafanya viongozi wawe wezi kwa kuwa wataanza kuhifadhi pesa nje ya nchi ili watakapomaliza uongozi wao ziweze kuwasaidia wakishakuwa wakimbizi kwenye nchi za watu" Sumaye.
"Wengine mna mahoteli makubwa, mabasi ya kusafiri kuliko hata haya mashamba yangu. siasa ni ushindani hivyo ni vyema kushindana kwa hoja kuliko visasi na kwenye hizi siasa za upinzani mnufaika mkubwa ni mwananchi kwamba atamchagua kiongozi anayemuhitaji" aliongeza.
Pamoja na hayo Mh. Sumaye amefunguka kuhusu utawala na kusema haelewi kama ni sheria zimebadilika au la kwani Spika wa bunge amekuwa akitoa maamuzi yake juu ya viongozi wa upinzani na kusema kuwa spika ni muwakilishi tu wa wabunge wote wala siyo mtoa maoni.
"Katika historia ya nchi hii tumeshuhudia jeshi la polisi lenye silaha likiingia ndani ya bunge na kupiga wabunge wetu pamoja na kuwatoa nje wabunge wasiokuwa na silaha hili jambo tumekuja kuona kwenye utawala wa awamu hii. Kuwachukulia hatua wabunge kisa wanabishana siyo sawa kwani ndiyo kazi yao. Siyo sahihi kupiga watu wanaopingana kwa hoja. Mhimili wa utawala kuingilia bunge ni kuwatisha wabunge wasiikosoe serikali" alimaliza Sumaye.
No comments