Ads

Simba waliamsha dude uhuru waipiga Ruvu goli saba

Dar/Mikoani. Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi amewajibu kwa vitendo wanaomwita 'mhenga' kwa kufunga mabao manne akiongoza Simba kuisambaratisha Ruvu Shooting kwa magoli 7-0 katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo unaifanya Simba kuongoza ligi kwa tofauti ya mabao kabla ya mabingwa watetezi Yanga kesho Jumapili kucheza na Lipuli kwenye Uwanja wa Uhuru.
Okwi aliyejiunga na Simba msimu ameanza kuonyesha ubora wake kwa kufunga mabao yake matatu katika dakika 45 za kwanza akimalizia pasi nzuri za kiungo Muzamiru Yassin kabla ya kuongeza moja katika kipindi cha pili akiunganisha pasi ya Said Ndemla. Mabao mengine ya Simba yalifunga na Shizza Kichuya, Juma Luizio na Erasto Nyoni.
Akizungumzia mabao yake Okwi alisema magoli hayo anayatoa kwa mke wake ambaye ni mjamzito na ndio maana alijituma sana katika mchezo huo ili kumpa zawadi nzuri mke wake kipenzi.
Okwi alianza kufungua karamu ya mabao ya Simba dakika ya 18 akifunga kwa shuti kali akimalizia pasi ya Mzamiru kabla ya kufunga la pili dakika ya 22 baada ya kumpiga chenga beki wa Ruvu Shooting,Shaibu Nayopa na kutumbukiza mpira nyavuni, na kisha kufunga tena la tatu dakika ya 35 kabla ya kuhitimisha siku yake nzuri ya jana kwa kufunga bao la nne dakika ya 53 akimalizia pasi ya Said Ndemla.
Mabao mengine ya Simba katika mchezo huo yalifungwa na Shiza Kichuya dakika ya 41 akimalizia pasi ya Erasto Nyoni kabla Juma Liuzio kufunga lingine dakika ya 45 na bao la saba likifungwa na Nyoni dakika ya 81 akimalizia pasi safi ya Said Ndemla.

Simba ilitawala mchezo huo katika vipindi vyote viwili huku Ruvu Shooting ikishindwa kupiga hata shuti moja  la maana golini kwa Simba  huku kocha wa maafande hao,Abdulmatic Haji Kiduu akijitetea kuwa wamefungwa kwa sababu ya kuwakosa wachezaji wake sita wa kikosi cha kwanza walio katika mashindano ya Majeshi nchini Burundi.
 Kama Simba ingekuwa makini ingeweza kufunga mabao mengi zaidi katika mchezo huo kwani dakika ya 21,Liuzio alishindwa kuipatia timu yake bao akipokea pasi safi ya mpira wa faulo kutoka kwa Haruna Niyonzima lakini akashikwa na kitete akishindwa kujua afunge au ampe pasi Okwi na kujikuta mpira wake ukiwahiwa na kipa wa Ruvu Shooting,Bidii Abdallah.
Pia Niyonzima alikosa bao dakika ya 36 akipokea pasi safi ya Liuzio lakini baade akatolewa kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Mohammed Ibrahim.
Katika mchezo huo wachezaji Mangasini Mangasini na Ishara Juma wa Ruvu Shooting walionyeshwa kadi za njano kwa kuwafanyia faulo Okwi na Niyonzima.
 Kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara, Azam iliichapa Ndanda bao 1-0 lililofungwa dakika ya 34 na mshambuliaji Yahaya Mohammed.
 Singida United pamoja na kufanya usajili mkubwa bado wamekalibishwa katika Ligi Kuu kwa kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mwadui kwenye Uwanja wa Mwadui Complex Shinyanga.
Paulo Nonga alianza kuipatia Mwadui bao dakika ya 30 baada ya kumchambua kipa wa Singida United,Manyika Peter na kutumbukiza mpira nyavuni kabla ya Kenny Ally kuisawazishia Singida United dakika ya 53 akimalizia pasi ya Atupele Greeen.
Salim Hamis aliipatia Mwadui bao la pili na la ushindi kwa kichwa dakika ya 64 akimalizia pasi ya Hassan Kabunda na kumuacha  kocha wa Singida United, Hans Pluijm ambaye aliushuhudia mchezo huo akiwa jukwaani kutokana na kutumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakati akiwa Yanga.
 Kwenye Uwanja wa Manungu Turiani Morogoro,Mtibwa Sugar iliichapa Stand United bao 1-0, shukrani kwa goli la Hussein Javu alilolifunga dakika ya 76, akimalizia krosi ya Issa Rashid'Baba Ubaya'.
Uwanja wa Sabasaba Njombe,Prisons iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji Njombe Mji.Mabao ya Prisons yalifungwa na Kassim Hamis na Nurdin Chona. 
Kwenye Uwanja wa  Uwanja wa Sokoine Mbeya wenyeji Mbeya City iliichapa Majimaji bao 1-0,bao la washindi likifungwa kiufundi na Eliud Ambokile dakika ya 32 baada ya kupokea mpira wa kurushwa kutoka kwa Hassan Mwasapili kisha kuutuliza kifuani na kuachia shuti kali nje kidogo ya 18 na mpira kumshinda kipa wa Majimaji Hushimu Mussa.
Kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba,wenyeji Kagera Sugar walilala kwa bao 1-0 dhidi ya Mbao, bao la washindi likifungwa dakika ya sita na Boniface Maganga.
Msimamo wa Ligi Kuu Bara
                                  P  W  D  L   F   A  Pts
1.Simba                       1    1   0  0  7   0    3
2. Prisons                    1    1   0  0  2   1     3
3.Mwadui                   1   1   0  0  2   1     3     
4.Azam                       1   1   0  0  1  0     3                
5. Mbao                      1   1  0  0  1   0    3       
6. Mbeya City             1   1  0   0  1  0    3
7. Mtibwa                   1   1   0  0  1  0   3      
8. Kagera                    1   0   0  1  0  1   0
9.   Ndanda                1   0   0  1  0  1   0               
10.  Stand                   1   0   0  1  0  1    0      
11.  Majimaji               1   0   0  1  0  1   0
12.  Njombe               1   0    0  1  1  2   0
13. Singida United         1    0   0  1  1  2  0        
14. Ruvu Shooting      1    0   0  1  0  7  0
 15. Lipuli                  0     0   0   0  0  0  0
16. Yanga                  0     0   0   0  0   0  0

No comments

Theme images by andynwt. Powered by Blogger.