Ads

OKWI BWANA AAMUA KUWAJAZA UPEPO SIMBA


Image result for okwi

 EMMANUEL Okwi juzi Jumapili aliifungia Simba bao lake la kwanza tangu ajiunge nao akitokea SC Villa ya kwao Uganda, lakini akakiangalia kikosi cha timu yake na kubaini kuwa bado hakijachanganya vema na kuwataka wenzake kupambana na hali zao.
Mganda huyo alifunga bao hilo sekunde chache kabla ya mapumziko ya mechi ambayo Simba iliicharaza Mtibwa Sugar bao 1-0 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ambapo baada ya mchezo huo alisema Simba bado sana.
Alisema kwa jinsi anavyoijua Simba na aina ya usajili uliofanywa na mabosi wao, ni wazi ingekuwa na moto mkali zaidi, akawataka wenzake kuamka ili Agosti 23 watakakapoivaa Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii wawape raha mashabiki wao.
Okwi alisema japo amegundua kuwa kikosi chao kinafanya makosa madogo madogo, lakini bado anaamini kama wakijiandaa vema wataipiga nyingi Yanga kama walivyoitia aibu Mei 6, 2012 walipoicharaza mabao 5-0 katika Ligi Kuu Bara.
Katika mchezo huo wa kufungia msimu huo wa 2011-2012 ambapo Simba ilitwaa taji lao la mwisho la Ligi Kuu Bara, Okwi alitupia mabao mawili, huku mengine yakifungwa na Felix Sunzu, Juma Kaseja na Patrick Mafisango.
“Kazi yangu ni kufunga, ila bado hii ni kazi ya ushirikiano wa timu nzima, naamini mwelekeo wa timu kwa ligi inayokuja utakuwa mzuri zaidi ya hapa, tofauti na sasa ambapo bado tuna makosa labda kwa vile hatujazoeana vizuri, kiasi cha kujua nani anataka ninii, ila ni lazima tujipange kwelikweli tuweze kutisha zaidi,” alisema.
Okwi aliwapa matumaini mashabiki kuwa mechi ya Ngao ya Jamii wataingia uwanjani ili kuwapa burudani na ushindi dhidi ya wapinzani na kuwahimiza wafike kwa wingi Uwanja wa Taifa kuona anachokifanya.
“Nguvu ya mashabiki ni kubwa na inatutia moyo, waje kwa wingi kuhakikisha timu yao inafanya kitu cha kipekee kama matarajio yao yalivyo, tukika sawa kwa maana ya kuelewana basi Yanga tunaweza kuwapiga nyingi tu,” alisema Okwi.
MAYANJA AKIRI
Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, amekiri kwamba bado kikosi chao hakijaelewana, hivyo wanafanyia kazi makosa yote ili timu ikae sawa kabla ya mechi yao ya Ngao ya Jamii.
“Wachezaji wakielewana ni imani yangu kwamba timu itakuwa vizuri zaidi, kuna makosa madogo yanafanyika, ila kila mchezaji anajituma kadiri awezavyo kuona anatoa mchango wake, naona juhudi zao, hilo litatupa mwelekeo mzuri,” alisema.
“Hatuwabezi Yanga, tunajua nao wanajipanga, ila kikubwa tunawajenga wachezaji wetu kuamini katika kujituma na hii ndio chachu ya ushindi.”     

No comments

Theme images by andynwt. Powered by Blogger.