Ads

MWAKIEMBE AVUNJA BMT RASMI....



Image result for mwakyembe

Dar es Salaam. Hatimaye Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ametangaza rasmi kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi na wajumbe wa Baraza hilo huku akitaja kasoro kadhaa za Baraza.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Waziri Mwakyembe alisema  baada ya agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Bungeni mjini Dodoma la kumtaka afanye mapitio na kuitathmini upya BMT ili kujiridhisha na usimamizi wake wa shughuli za michezo nchini limekuja wakati muafaka.
"Miongoni mwa changamoto zinazolikabili Baraza hilo na hali ya uhuria uliopitiliza katika uongozi na uendeshaji wa michezo karibu yote nchini.
"Pamoja na BMT kulalamikia uhaba wa fedha kuwa kikwazo kikubwa kinachokwamisha  utendajikazi wake, Wizara ililiona zaidi hitaji la utashi, dhamira na kujituma kuliko pesa katika kutatua sehemu kubwa ya udhaifu  uliotamalaki tasnia ya michezo.
"Mifano michache ni pale viongozi wa michezo kushika zaidi ya nafasi moja ya uongozi tena kwenye mchezo mmoja, ushiriki wa wanamichezo wa Tanzania nje ya nchi bila kuitaarifu BMT, mapromota wa mchezo wa ngumi nchini kuendesha shughuli zao bila kusajiliwa, chaguzi za vyama vya michezo kugubikwa na ubabe na rushwa, katiba na kanuni za vyama vya michezo kukosa uhakiki kubaini upungufu kuhusu masuala ya fedha;, tuhuma za rushwa, ubadhirifu, upendeleo, maamuzi ya kibabe ya wazi kabisa kutofuatiliwa na kufanyiwa kazi ni baadhi tu."
Waziri huyo alifafanua kwamba BMT ambayo imeundwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge Na.12 ya mwaka 1967 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 1971, jukumu lake kubwa ni kuendeleza michezo, lakini  kwa kipindi kirefu tasnia ya michezo imegubikwa na migogoro ya mara kwa mara ambayo imechangia sana kudumaza maendeleo ya michezo katika nchi yetu. Serikali ya Awamu ya Tano ilitarajia kwamba kupitia BMT, migogoro hiyo ingeweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
"Kwa mujibu wa Sheria iliyoanzisha BMT, Baraza limepewa jukumu la kushughulikia masuala yote yanayohusu michezo ikiwa ni pamoja na weledi, amani, utulivu na utawala bora katika tasnia ya michezo.
Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wajumbe wote wa BMT kwa jitihada waliyofanya kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza toka wateuliwe mwaka 2015," alisema Waziri Mwakyembe huku akifafanua kwamba.
"Kwa kuzingatia kasi ya mageuzi ya Serikali ya Awamu ya Tano na matarajio ya haraka waliyonayo wananchi kuiona tasnia ya michezo ikionesha tija, nimeamua kwa mamlaka niliyopewa na Sheria ya BMT na.12 ya 1967 (kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria Na.6 ya 1971) pamoja na Kanuni zake za 1999, kusitisha uteuzi wa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wote wa BMT kuanzia leo  na Sekretarieti ya Baraza itaendelea kufanyakazi katika kipindi hiki," alimaliza.

No comments

Theme images by andynwt. Powered by Blogger.