KWA HILI JEMBE LA YANGA LAZIMA MULIKUBALI
SHIZA Kichuya alijipatia umaarufu mkubwa msimu uliopita kwa bao lake la kideoni alilomtungua kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ na kuisawazishia Simba bao katika pambano dhidi ya Yanga, lakini sasa Simba lazima wake chonjo.
Yanga imeleta beki shupavu wa kati kutoka Nigeria ambaye zinahesabiwa siku kabla ya kumwaga wino. Jamaa ni mbaya kwa mipira iliyokufa na fundi wa kutupia kambani mipira iliyochongwa kona, huku akiwa na sifa ya kupiga kwa miguu yote miwili.
Beki huyo ni Henry Tony Okoh anayewania nafasi moja ya nyota wa kigeni iliyosalia Yanga sambamba na kiungo Mkameruni, Fernando Bongyang.
Jamaa huyo bwana, kwa mipira ya mguu wa kushoto ni mzuri, huko kulia ndio usiseme na kama Yanga itamsainisha mkataba wa kuitumikia timu hiyo ni vema nyota wa Simba na timu nyingine za Ligi Kuu Bara wasijaribu kabisa kutoa mipira ya kona.
Mwanaspoti limefanya mazungumzo na beki huyo na kufunguka mambo mengi ikiwamo umahiri wake wa mipira iliyokufa na kufunga kwa vichwa.
ALIVYOIJUA YANGA
“Kwanza niseme wazi sikuwa naijua Yanga kabisa, ni meneja wangu ndiye aliyeniambia kuna timu inaitwa Yanga na inahitaji mchezaji wa kiwango changu, hapo ndipo nikaanza kuifuatilia ili niifahamu vizuri,” anasema Henry kwa Kiingereza kama cha wale waigizaji wa sinema za Nollywood, lakini yeye akijitahidi kuchanganya na neno moja moja la Kiswahili kujizoesha na maisha mapya ya Bongo.
“Nashukuru baada ya kuanza kufuatilia habari zake, nikagundua kuwa hii ni moja ya klabu zenye majina makubwa si hapa tu, hata Afrika.”
TIMU ALIYOTOKA
Akizungumzia alikokuwa kabla ya kuja Tanzania, anasema alikuwa akiichezea Lagos Athletic ya kwao Nigeria aliyoitumikia msimu mmoja tu, alijiunga na timu hiyo akitokea Akwa United anayosema alidumu nayo kwa misimu minne baada ya kuibukia soka la juu la huko kwao.
MAFANIKIO YAKE
“Kuhusu mafanikio yangu naweza kusema labda ni kucheza timu ya taifa ya vijana ya umri chini ya miaka 23. Nilifanya hivyo misimu miwili iliyopita, unajua Nigeria kuna wachezaji wengi, hivyo kupata nafasi kama hiyo si jambo dogo,” anasema.
“Lakini kwa ngazi ya klabu, nimewahi kutwaa tuzo ya beki bora mara mbili nikiwa Akwa United. Tuzo hiyo ilinipatia nafasi ya kusajiliwa Cyprus kabla ya kurudi nyumbani na kuichezea Akwa tena, kisha ndio nikajiunga na Lagos Athletic.”
AHADI ZAKE JANGWANI
“Nitapambana kukamilisha ndoto zangu. Sitaki kukaa sana Yanga, nataka kufika mbali zaidi. Kama nilivyokwambia, Nigeria wanasoka tupo wengi mno, nimeona nije Yanga ili nipate kuonyesha uwezo wangu kwa kuisaidia klabu hii, lakini hapo hapo niweze kujitangaza, nataka kufika mbali,” anaongeza Henry.
“Najua hapa (Yanga) ni rahisi kujitangaza zaidi kimataifa na kuonyesha nilicho nacho hasa kwa kuwa klabu hii inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika. Naamini nipo katika timu sahihi ya kutimiza malengo yangu.”
KINACHOSUMBUA BONGO
Hana muda mrefu tangu awasili nchini, lakini jambo lililoanza kumsumbua kwa haraka ni chakula.
“Chakula bwana. Chakula chenu kinanipa wakati mgumu sana, kweli hapa kuna baadhi ya vyakula ambavyo hata kwetu vipo. Tatizo ni namna vinavyoandaliwa,” anasema.
“Kwetu tuna wali maharage pia, lakini wali wa hapa umenishinda. Sina budi kujilazimisha hivyo hivyo kwani ndicho chakula pekee ninachokiweza, vingine vimenishinda.”
JEZI NYEKUNDU
Wahenga walisema ‘Usilolijua ni usiku wa giza’. Unajua nini, Mnigeria huyu kwa ugeni wake aliwahi kuvaa jezi nyekundu pale Yanga, kilichomtokea sasa, anasema kutokisahau.
“Kama nilivyosema, nilikuwa siijui Yanga na hii ni mara yangu ya kwanza kuja Tanzania. Sasa siku moja nilivaa jezi nyekundu ili niingie mazoezini, nakumbuka ofisa mmoja alinirudisha chumbani haraka akiniambia nguo nyekudu ni mwiko kabisa klabuni hapa, akaniamuru nirudi hotelini kubadilisha,” anasema Henry.
“Nilishangaa sana, baadaye nilipotulia nilimuuliza mmoja wa wachezaji wenzangu akaniambia ukiwa Yanga hauruhusiwi kuvaa jezi wala fulana nyekundu na ukiwa Simba nako hautakiwi kuvaa nguo ya njano wala kijani. Ndio nikajua kumbe!”
VIPAJI YANGA
“Yanga ni timu nzuri kulingana na aina ya wachezaji waliopo hapa, unajua mpaka sasa nilivyokaa nao kitu pekee nilichokiona kinapungua ni wachezaji wengi hawana nguvu, lakini angalia yule mshambuliaji anayevaa jezi namba 10 mazoezini (Ajibu) ni mtu hatari sana, yaani ili beki ukabiliane naye lazima jasho likutoke. Hapa mazoezini tu tunamkoma, sasa sijui huko kwenye ligi,” anasema Mnigeria huyo.
NAFASI YAKE
“Kwa sasa ninachofanya ni kufuata maelekezo ya kocha ni kipi anataka kukiona, sina wasiwasi na kipaji changu hasa nikiangalia kiwango cha mabeki waliopo hapa Yanga, nasubiri majibu ya kocha atakavyoamua, nafikiri tusubiri,” anasema kwa kujiamini.
UBORA WAKE
“Nafasi yangu ni beki wa kati. Nikicheza hapo najua namna ya kukabiliana na washambuliaji, huwa sikubali mshambuliaji afunge kupitia kwangu. Ninachofanya ni kumuwahi straika kabla hajaleta madhara katika lango letu,” anasema Henry ambaye mazoezini ameonyesha pia uwezo wa kufunga kwa mipira ya adhabu hasa kutokea maeneo ambayo yanapasa kutumia mguu wa kushoto, pia anajua kufunga kwa kichwa.
Anasema katika Ligi ya kwao amefunga zaidi ya mabao 10 kwa vichwa hasa mipira inayotokana na kona na faulo, kitu ambacho anaamini atakiendeleza hata atakapotua Yanga.
No comments