HAYA HAPA MANENO YA HAJI MANARA BAADA YAKUTOKA KIFUNGONI
Leo ni Siku kubwa kwa mchezo wa mpira wa miguu nchini hususan washabiki na mchezo huo murua, baada ya kamati ya nidhamu kuitengua adhabu yangu ya kufungiwa mwaka mmoja,kujihusisha na maswala ya kandanda ndani na nje ya nchi.
Adhabu hii ilikuwa inaiumiza sana klabu yangu na kuiondolea haki yake muhimu, ya kuwapa habari kwa wakati watanzania juu ya kinachoendelea kwenye Club.
Kiukweli niishukuru kamati ya nidhamu chini ya Mwenyekiti wake Tarimba Abbas kwa kuiondoa adhabu hii, kiukweli alioondolewa adhabu sio Haji, ni Simba na mchezo wenyewe wa Soka.
Hakika hawa wamesikia kilio cha wengi, na kilio cha wengi kina nguvu ya Mungu Mwenyezi, Shukran kwa Mola kwa kuwapa nguvu hii kina Tarimba na wenzake.
Niwashukuru pia viongozi wa TFF kwa utashi wao kwenye hili.
Nitakuwa mjinga nisipowashukuru wanasimba wenzangu ambao siku zote wamekuwa upande wangu, hawa ninawaahid kuwatumikia kwa moyo na dhamira ileile ya Haji ya kuhakikisha haki na wajibu wetu kama klabu unatekelezwa.
Kipekee niwashukuru viongozi wangu wa Simba ambao walihakikisha jambo hili linapatiwa ufumbuzi wa haraka na linamalizika kwa njia ya amani.
Mwisho
niwashukuru watu wote mliokuwa nami katika sala na dua zenu,hususan kwenye kipindi kigumu cha adhabu.
Sitapenda kufukua makaburi, yatupasa sote tusonge mbele, hakuna aliyeshinda, umeshinda mchezo wa soka.
Nawaahidi kuendelea kufanya kazi zangu kwa weledi,nidhamu na kwa kuzingatia miiko ya mchezo huu unaobeba dhamana za maisha ya watu walio wengi, sambamba na kuendelea kuitetea na kuilinda klabu yangu kwa nguvu zote.
No comments