Umisseta yaleta neema kwa wafanyabiashara....
Mwanza.Waswahili wanasema mgeni njoo mwenyeji apone, ndiyo kinachotokea kwa sasa katika mashindano ya Umisseta baada ya wafanyabiashara ndogondogo kumiminika kwenye Viwanja vya Chuo cha Ualimu Butimba jijini, Mwanza.
Wafanyabiashara hao wa matunda na bidhaa ndogondogo wanachekelea jinsi wanafunzi wanavyonunua vyakula na vinywaji katika maeneo hayo.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wafanyabiashara hao wameanza kuomba dua ili hata msimu ujao mashindano hayo ya Sekondari (Umisseta) yafanyike tena mkoani hapa.
Bakari Soud anayeuza maji, miwa na matunda alisema mashindano hayo kuwapo Mwanza yamekuwa faraja kwake kwani riziki zinapatikana na maisha yanakwenda.
Soud alisema naomba sana dua mashindano hayo yaendelee kuwapo na kufanyika katika jiji la Mwanza kila mwaka ili tufanye biashara.
“Kwa ujumla sikufuru, riziki zinapatikana hii ni fursa pekee ambayo wafanyabishara kama sisi tunafurahi sana kuwapo kwa mashindano haya... naomba sana dua ili hata mwakani yarudi tena,” alisema Soud.
Naye Amani Josiah anayeuza vyakula alisema kuwa hii fursa hawezi kuisahau kwani biashara yake inaenda vizuri na wanafunzi ameshawabaini vyakula wanavyopendelea.
Alisema kutokana na hali hiyo vitu vidogovidogo kama barafu, bisi (mahindi ya kukaanga), maembe na machungwa lazima awe navyo kwani wanafunzi wanapenda sana.
“Hii ni fursa kwakweli tunashukuru kwa mashindano haya kuwapo Mwanza, kwangu vyakula kama bisi, chipsi vinapendwa sana na wanafunzi,” alisema Josiah.
mwanaspoti
No comments