SportPesa yaingilia kuokoa jahazi Yanga....
YANGA bado ina hali ngumu kifedha. Ni ukweli ingawa hauwaingii akili kirahisi mashabiki wa timu hiyo ambao wameanza kushtuka hasa baada ya mastaa kadhaa kutua Jangwani wakapiga picha na viongozi lakini wakaenda kusaini kwenye klabu pinzani za Simba na Azam.
Kampuni tajiri ya SportPesa ambao ni wadhamini wapya wa Yanga, imeingilia kati hali kiuchumi ndani ya klabu hiyo na kuokoa jahazi.
Viongozi wameingia makubaliano maalum na wadhamini hao wakakopeshwa fungu ambalo limetumika kulipa malimbikizo yote ya mishahara na kila mchezaji na mfanyakazi wa Yanga sasa roho kwatu.
Sportpesa wamekubaliana kwa siri na vigogo wa Yanga kwamba kwenye fungu hilo walilokopeshwa la Sh400 milioni watakatana juu kwa juu ili mradi mambo yaende sawa na vijana warudi kwenye morali yao na sasa wanajipanga kupata vyanzo vingine tayari kwa usajili mpya ambao Simba wanaufanya kwa fujo kweli kweli.
MASTAA WABEBWA
YANGA
Viongozi wa Yanga walimpeleka straika John Bocco kwa Kocha George Lwandamina, akampotezea, Simba wakambeba. Kocha huyo akawaambia viongozi kwamba anamtaka beki wa kushoto wa Mbao, Jamal Mwambeleko wakamwita Dar es Salaam na kumpa maneno mengi na tarehe ya kumalizana naye, Simba wakaingilia kati wakamalizana naye fasta wakampa chake akatia mfukoni akalala mbele.
Wakati Yanga wakishangaa picha za Mwambeleko kusaini Simba kwenye gazeti la Mwanaspoti, wakatumiwa picha kwenye Whatsapp kwamba yule mshambuliaji Waziri Junior wa Toto aliyekuja klabuni hapo jana yake akapiga picha mpaka na makombe na kuwahakikishia yeye ni mali ya Yanga, kasaini Azam waliompa Sh10 milioni tu.
Vigogo wengi maarufu ndani ya Yanga baada ya kuona hali ya kiuchumi haieleweki wamekuwa wakijiweka mbali na usajili huo kwa kuogopa kuchafuka na kupoteza sifa mbele ya mashabiki, ingawa ukweli ni kwamba bado wamo na wanamsikilizia Mwenyekiti, Yusuf Manji.
WAZIRI AFUNGUKA
Waziri Junior baada ya kusaini Azam ameweka wazi kile kilichomkimbiza kuingia mkataba na mabingwa wa soka nchini Yanga na kutua Azam ambapo ametamka kwamba hawakuwa siriazi na maneno yalikuwa mengi kuliko vitendo ambavyo haviendani na hali halisi.
Waziri ambaye ametokea Toto African ya jijini Mwanza iliyoshuka daraja alisaini mkataba wa miaka miwili na Azam FC akitokea kuwasikiliza Yanga ambao alishawahakikishia kwamba wasiwe na wasiwasi.
“Yanga walikuwa wa kwanza kuzungumza nami, Azam wamefuata, nilikwenda pale Yanga kuzungumza nao lakini wanaonekana ni watu wenye maneno mengi, sielewi tatizo ni nini ndiyo maana niliona ni vyema niende Azam ambako pia walikuwa wanahitaji huduma yangu.
“Ni kweli Yanga wanashiriki mashindano makubwa lakini ushiriki wao kwangu haunisaidii kitu chochote naangalia maisha, kama kushiriki michuano mikubwa sioni maana kwani wanaenda na wanarudi bila faida, hivyo nimefanya uamuzi sahihi ambao nimeuamua mwenyewe bila kushinikizwa na mtu,” alisema Waziri Jr.
CHANONGO
NI YANGA
Yanga walipanga kumtumia kiungo wa Mtibwa Sugar, Haroun Chanongo kwenye michuano ya Sportpesa Super Cup lakini baadaye ilidaiwa kuwa mchezaji huyo alizuiwa kucheza mechi hiyo kwani hakuwa na leseni ya usajili.
Baada ya kuwepo na sintofahamu hiyo kutokana na watani zao Simba kuwatumia wachezaji wengine ambao hawajasajiliwa, Chanongo ameamua kuweka wazi kuwa alifuatwa na viongozi wa Yanga kwa ajili ya usajili wa msimu ujao wa ligi kuu na si mashindano hayo.
Chanongo aliliambia Mwanaspoti kuwa alizungumza na Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa ambaye alielezea shida yao kuwa ni kuhitaji huduma yake kwa msimu ujao na si kwenye mashindano hayo.
“Mimi nilipigiwa simu na Katibu wa Yanga, Mkwasa ila alichonieleza ni kwamba wanaomba huduma yangu msimu ujao kwa maana ya kunisajili kwenye mechi za Ligi Kuu na siyo haya mashindano, baada ya siku kadhaa nilishangaa kusikia kuwa nitaichezea Yanga kwenye Sportpesa Super Cup,” alisema.
“Katibu alisema jina langu litapelekwa kwenye Kamati ya Usajili hao ndiyo watanipigia simu hivyo nasubiri wanipigie, mkataba wangu ni wa miaka miwili na Mtibwa lakini upo wazi na ndiyo maana nilichukuwa pesa ya usajili ya mwaka mmoja, kwa makubaliano kwamba nikipata timu niwe huru kuondoka ama nikiridhika na mazingira ya hapa basi nilipwe pesa iliyobaki, nashukuru nimejitahidi kufanya vizuri na Mtibwa.”
chanzo, mwanaspoti...
chanzo, mwanaspoti...
No comments