Mkenya David Rudisha ashindwa mbio za China............
Bingwa mara mbili wa michezo ya Olimpiki mbio za mita 800 David Rudisha ameanza vibaya msimu mpya wa riadha huko China Jumamosi lakini Wakenya wenzake Faith Kipyegon na Hellen Obiri wakaibuka washindi kwenye mbio zao.
Akishiriki katika mkondo wa pili wa mfululizo wa mashindano ya Golden League, Rudisha, ambaye anashikilia rekodi ya dunia, alimaliza wa nne kwa muda wa dakika moja, sekunde 45, nukta 36.
Wakenya wenzake walichukua nafasi tatu za mwanzo wakiongozwa na Kipyegon Bett kwa dakika moja, sekunde 44, nukta 70 akifuatiwa na Robert Biwott na Ferguson Rotich.
Hatimaye Rudisha amesema matokeo hayo mabovu ni kwa sababu hajakimbia kwa muda mrefu tangu mwaka jana aliposhinda dhahabu yake ya pili katika michezo ya Olimpiki mjini Rio de Janeiro.
``Sijafurahishwa na matokeo hayo lakini sasa nitajua ni wapi nitarekebisha. Nimefanya mazoezi ya kutosha kwa hivyo nina uhakika wiki chache zijazo nitakuwa sawa,'' amesema Rudisha.
Bingwa wa Olimpiki mbio za mita 1,500 Faith Kipyegon aliibuka mshindi kwa muda wa kasi zaidi msimu huu wa dakika tatu, sekunde 59, nukta 22, wa pili na wa tatu wakawa ni wanariadha wa Ethiopia Dawitt Seyaum na Basu Sado.
Katika mbio za mita 5000 Hellen Obiri, mshindi wa medali ya fedha michezo ya Olimpiki ya Rio, naye pia aliwaangusha wanariadha wa Ethiopia, Senbere Tefere na Letesenbet Gidey waliochukua nafasi ya pili na ya tatu mtawalia.
Obiri alikimbia kwa muda wa dakika 14, sekunde 22 nukta 47 na kutangaza nia yake ya kunawiri katika mbio za dunia mwezi Agosti mjini London mwaka hu.
Bingwa wa Olimpiki mbio za mita 100 za wanawake Elaine Thompson wa Jamaiza alishinda kwa muda wa kasi zaidi duniani msimu huu, sekunde 10 nukta 78.
No comments