Meli ya kivita Japan kusindikiza meli ya Marekani.............
Japan imetuma meli ya kubwa zaidi ya kivita baharini, hatua yake ya kwanza ya aina hiyo tangu kupitishwa kwa sheria mpya yenye utata iliyowezesha taifa hilo kuanza kupanua uwezo wa jeshi lake.
Meli hiyo kubwa ya kubeba helikopta ambayo imepewa jina Izumo imetumwa kuifuata meli ya kubeba mizigo na vifaa vya kijeshi ya Marekani ambayo inapitia katika maeneo ya bahari ya Japan.
Meli hiyo ya Marekani inaelekea kufikisha mafuta kwa meli nyingine za taifa hilo zinalohudumu eneo hilo, ikiwemo meli yake kubwa ya kubeba ndege ya Carl Vinson na meli zinazoandamana na meli hiyo karibu na rasi ya Korea.
Korea Kaskazini imetishia kuizamisha Carl Vinson pamoja na nyambizi ya Marekani, huku wasiwasi ukiendelea kuongezeka eneo hilo.
- Kombora jingine la Korea Kaskazini lafeli majaribio
- China 'yaeleza wasiwasi' kuhusu Korea Kaskazini
- Marekani: Korea Kaskazini ilikusudia uchokozi
Aidha, taifa hilo lilifanya jaribio la kurusha kombora ambalo lilifeli Jumapili, licha ya kuonywa mara kadha na Marekani na nchi jingine dhidi ya kufanya majaribio ya makombora au majaribio ya silaha za nyuklia.
Mwandishi wa BBC Rupert Wingfield-Hayes aliyepo mjini Tokyo anasema Izumo ndiyo ambayo ni fahari ya jeshi la wanamaji la Japan, na kufikia sasa ndiyo meli kubwa zaidi ya jeshi hilo.
Izumo ina urefu wa mita 249 na inaweza kubeba helikopta hadi tisa.
Inafanana sana na meli za kivita za kushambulia adui majini za Marekani ambazo zinamilikiwa na Marekani, gazeti la Japan Times linasema.
Shirika la habari la Kyodo limesema meli hiyo imeondoka kwenye kambi yake eneo la Yokosuka kusini mwa Tokyo kwenda kuungana na meli hiyo ya kusafirisha bidhaa za jeshi la Marekani, na kwamba itaisindikiza hadi kwenye pwani ya Shikoku magharibi mwa Japan.
Chini ya Waziri Mkuu Shinzo Abe, Japan inaanza kujiimarisha kijeshi kufikia kiwango ambacho inaruhusiwa kimataifa, na huku wasiwasi ukiongezeka katika rasi ya Korea, bw Abe anaonekana kuwa makini sana kujaribu kutumia sheria mpya zinazoikubalia serikali kuimarisha jeshi la nchi hiyo kwa mara ya kwanza, mwandishi wetu anasema.
Katiba ya baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia huzuia jeshi la Japan dhidi ya kutumia nguvu za kijeshi kutatua mizozo, ila tu wakati wa kujilinda.
Izumo ndiyo meli ya kwanza ya kivita vya Japan kutumwa kwenye shughuli rasmi, ambayo si ya mazoezi, tangu kupitishwa kwa sheria mpya mwaka 2015 ambayo inaipa idhini Japan kusaidia washirika wake wanaposhambuliwa.
Serikali ya Bw Abe, ambayo ilipigania mabadiliko hayo ya kikatiba, imekosolewa kwamba sheria hizo mpya huenda zikaitumbukiza Japan kwenye migogoro na vita visivyofaa nje ya nchi hiyo.
Bw Abe amekanusha shutuma hizo.
Kutumwa kwa Izumo kumejiri baada ya mazoezi ya pamoja ya kijeshi yaliyofanywa na Japan na Marekani, pamoja na shughuli nyingine za majeshi ya majini.
Meli ya kutekeleza mashambulio baharini ya Ufaransa iliwasili kusini magharibi mwa Japan Jumamosi kwa mazoezi ambayo yatashirikisha majeshi ya majini ya Japan, Marekani na Uingereza.
No comments