Marekani yathibitisha haitosita kuidhibiti Korea Kaskazini.........
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson amesema Ijumaa kuwa Washington haitosita kuchukua hatua za kijeshi kwa vitendo vya uchokozi vya Korea Kaskazini na itaendelea kushinikiza kutengwa kwa taifa hilo la kidikteta kifedha na kimataifa.
“Kama tulivyosema awali, njia zote mbadala kwa kujibu uchokozi wake siku za usoni lazima zitakuwepo,” Tillerson ameuambia mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati akijadili suala la nyuklia la Korea Kaskazini.
“Vikwazo vya kidiplomasia na kiuchumi vitasaidiwa na azma ya kupambana na uchokozi wa Korea Kaskazini na pia kuchukua hatua za kijeshi ikilazimika kufanya hivyo,” ametahadharisha.
“Tunapendelea sana ufumbuzi wa tatizo hili kupitia mazungumzo, lakini tuko tayari kujilinda na washirika wetu dhidi ya uchokozi wa Korea Kaskazini.
Tillerson amesema kampeni hii mpya inayowekewa shinikizo itatekelezwa mara moja na kuathiri maslahi ya Korea Kaskazini,” lakini amesisitiza kuwa mapinduzi sio sehemu ya mkakati huo.
Ameongeza kuwa mazungumzo hayawezi kufanyika mpaka pale Korea Kaskazini itapochukua hatua za kuharibu programu yake ya kutengeneza silaha haramu.
Tillerson ameeleza kile ambacho Washington kinataka jumuiya ya kimataifa kifanye kuzuia Korea Kaskazini kufikia azma yake ya silaha za nyuklia, ikitaka kuwepo shinikizo zaidi la kidiplomasia na kiuchumi dhidi ya Pyongyang ili ibadilishe mwelekeo wake, pamoja na kuwekewa vikwazo maalum vipya.
“Ni lazima tuweke shinikizo la kiuchumi la juu kabisa kwa kusitisha mahusiano ya kibiashara ambayo yanaendelea kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika kuendelea kuwekeza katika programu ya nyuklia na makombora ya Jamhuri ya watu wa Korea Kaskazini.
“Natoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusitisha mtiririko wa wafanyakazi wa kigeni wa Korea Kaskazini na kuweka vikwazo juu ya biashara inayoingia kutoka Korea Kaskazini na hasa mkaa wa mawe.”
Aidha ameitaka hasa China kuongeza shinikizo juu ya Korea Kaskazini kwa kutumia nafasi yake ya kiuchumi.
Amezitaka nchi kupunguza mahusiano ya kidiplomasia na Pyongyang and kutekeleza kikamilifu maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na Korea Kaskazini.
“Yale mataifa ambayo hayajatekeleza maazimio hayo kikamilifu yanalichafulia sifa yake baraza hili,” amesema Tillerson.
“Kwa miaka mingi, Korea Kaskazini imekuwa ikiweka masharti ya mpango wake hatari unaoendelea wa kutengeneza silaha; ni wakati mwafaka sote kwa pamoja kuchukua hatua nyingine tena kudhibiti hali hii,” ameongeza Tillerson.
Marekani imeitisha mkutano wa Ijumaa ikiwa ni sehemu ya jukumu lake ikiwa ni rais wa Baraza la Usalama mwezi huu. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Tillerson kuhudhuria kikao hicho katika taasisi ya kimataifa na ofisi ya Baraza la Usalama iliokuwa imefurika wanadiplomasia wakati mataifa yakiwa na hamu kupata fununu kutoka utawala wa Trump ni wapi inaelekea kuhusiana na suala hatarishi la Korea kaskazini.
No comments