Kiongozi wa upinzani Zambia Hichilema ashtakiwa
Kiongozi wa upinzani nchini Zambia Hakainde Hichilema pamoja na naibu wake wamefikishwa mahakamani nchini humo ambapo wameshtakiwa makosa ya uchochezi wa maasi pamoja na kufanya mkutano kinyume cha sheria.
Wote wamekanusha mashtaka hayo, na wakaachiliwa huru kwa dhamana.
Mwandhishi wa BBC Meluse Kapatamoyo anasema wawili hao walitakiwa kulipa dhamana ya $2,500 (£2,000) kila mmoja na wanatarajiwa kurejea kortini tarehe 19 Oktoba.
Bw Hichilema alipakia picha zake akiwa kortini siku hiyo ya Alhamisi kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Bw Hichilema na naibu wake Geoffrey Bwalya Mwamba walikamatwa Jumatano na wakalala seli.
Mashtaka hayo yanahusiana na hotuba ya kushtukiza ambayo Bw Hichilema aliitoa 26 Septemba katika mji wa Mpongwe, katikati mwa nchi hiyo, shirika la habari la Reuters limesema likinukuu maafisa wa polisi.
Bw Hichilema alishindwa kwenye uchaguzi wa urais mwezi Agosti na Rais Edgar Lungu ingawa amelalamika kwamba kulitokea udanganyifu.
Juhudi zake za kutaka mahakama ibatilishe matokeo hayo ziligonga mwamba.
Aliandika kwenye Facebook Alhamisi: "Kukamatwa kwetu hakutatuzuia kutumia njia nyingine kutafuta haki kuhusu uchaguzi huu ambao tulipokonywa ushindi."
No comments