KAMA BOSSOU ANACHEZA TOGO, MROKI, MAGULI, LIUZIO KWANINI WANAACHWA STARS?
WAKATI fulani, Vicent Bossou alitemwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Togo lakini kazi yake nzuri klabuni Yanga SC ikamrejesha katika timu yake ya taifa na siku ya jana Jumapili mlinzi huyo wa kati mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya ushambuliaji alifunga goli la kwanza lililofungua matumaini ya Togo kufuzu kwa CAN 2017.
Ndiyo, Bossou yule aliyekuwa msugua benchi na kuitwa garasa atakuwa miongoni mwa wachezaji wanaocheza ligi kuu Tanzania Bara (VPL) ambao wataonekana katika fainali za mwakani za Mataifa ya Afrika.
Mlinzi wa kati raia wa Uganda, Juuko Murish pia atakuwa katika kikosi cha Uganda ambacho kimefuzu kwa michuano hiyo ya Gabon mapema mwaka ujao. Ni jambo zuri kuona VPL ikiwakilishwa katika michuano hiyo mikubwa ya kandanda barani Afrika.
Upande mwingine ni funzo ambalo makocha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars wanapaswa kujifunza. Tanzania katika miaka ya karibuni imekuwa na wachezaji rasmi wanaocheza ng’ambo.
Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Hamis Mroki, David Naftal, Juma Ndanda Liuzio, Uhuru Suleimani, Abdulhalim Humud, golikipa, Juma Mpongo, Elius Maguli na wengine wengi.
Ni kweli, Samatta na Ulimwengu wamekuwa na mafanikio tangu wangali wachanga na uwezo wao umekuwa machoni mwetu kuushuhudia, si rahisi kwa kocha wa timu ya Taifa, Charles Mkwasa kuwaacha kikosini, na inapotokea Ulimwengu au Samatta wakaachwa katika uteuzi, Mkwassa amekuwa akielezea sababu za kutowajumuhisha.
Ila tangu Maguli aliposajiliwa huko Oman hajawahi kuitwa kikosini, na wala kocha Mkwasa hajawahi kuweka wazi sababu za kutomuita mshambulizi huyo.
Mara ya mwisho Liuzio kuitwa kikosini ilikuwa miezi kumi iliyopita kutokana na majeraha lakini tangu mwezi April mwaka huu mshambulizi huyo amekuwa akicheza bila maumivu klabuni kwake Zesco United.
Mkwasa ni mtu mwenye dharau pengine, kwa maana unapowaacha wachezaji kama Maguli au Liuzio katika uteuzi bila kutuambia sababu ni makosa kwa kocha makini. Yeye amekuwa mwepesi kuelezea matatizo ya Samatta ama Tom na kusema sababu za kutowaita.
‘Ulimbukeni mtupu,’ na ukiritimba huo uliopo katika uteuzi wa kikosi cha timu ya Taifa mara kwa mara umekuwa ukiwaacha nje ya timu vijana wengi wa Kitanzania wanaocheza nje ya nchi, huku wakiwa na hamu kubwa ya kuiwakilisha timu yao ya Taifa.
Kama, Togo imekuwa ikimtumia Bossou anayecheza VPL ni kwanini Mkwassa anashindwa kuwajumuhisha vijana wenye uraia wa Tanzania wanaocheza ng’ambo.?
Mfano, Mroki, bahati nzuri huyu ni zao la Tanzania Soccer Academy -TSA na alikuwa sehemu ya timu ya Taifa ya vijana mwaka 2011, tena kama nahodha. Mroki amekuwa akicheza soka katika timu ya Kabin inayocheza ligi kuu ya Thailand na huko amekuwa akifanya vizuri tu.
Naftal yuko Kenya kwa miaka mitano sasa na amekuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza katika klabu yake lakini tangu alipoondoka Simba SC amekuwa ‘akiisikia kwenye bomba tu’ timu yake ya Taifa. Kama tatizo ni ligi na mahali wanapocheza mbona sasa Togo imekuwa ikimtazama Bossou katika timu yao ya Taifa wakati anacheza katika ligi ya kawaida-VPL.?
Watanzania wamekuwa wakiwashauri wachezaji wa hapa kupambana kucheza soka nje ya nchi. Kwanza ni kwa ajili ya kutengeneza maisha yao lakini pia wamekuwa wakiamini kitendo cha Watanzania kucheza nje kitakuwa na msaada wa ndani ya uwanja hadi katika timu ya Taifa.
Hakuna game isiyo na umuhimu, licha ya kwamba zipo mechi za kukamilisha ratiba. Naamini Mkwasa alipaswa kuwajumuhisha kikosini, Naftal, Mroki, Maguli, Liuzio na wengineo katika game vs Nigeria ili kujua wachezaji hao wana kitu gani kipya, lakini ‘amekuwa mbinafsi’ na hana mtazamo wa mbele kuhusu timu anayoisimamia.
Kama Bossou anacheza Togo, Mroki, Maguli, Liuzio kwanini wanaachwa Stars? Mwambieni Mkwassa aache ukiritimba, ajifunze kwa Bossou.
No comments