Ads

‘Waislamu acheni kujihusisha na maandamano yoyote nchini’.......


WAISLAMU nchini wametakiwa kuacha kujihusisha katika maandamano yoyote, ambayo yanaonekana kuhatarisha amani.

Badala yake, wamehimizwa wajielekeze kufanya kazi kwa bidii na kutafuta elimu ili kujiletea maendeleo.

Hayo yamesemwa na Imamu Mkuu wa Masjid Swalihina, Sheikh Mussa Chamwenyewe wakati akitoa hotuba ya swala ya Ijumaa katika msikiti huo uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Chamwenyewe alisema Waislamu hawatakiwi kuwa wa kwanza, kujihusisha kwenye vurugu na maandamano yoyote, ambayo yanaonekana kuhatarisha amani iliyopo nchini, badala yake wajikite katika kutafuta elimu na kufanya kazi kwa juhudi, jambo ambalo litakuwa na manufaa kwao.

Imamu huyo alisema kuwa kumejitokeza tabia ya baadhi ya Waislamu nchini, kushiriki katika maandamano yasiyo na tija, badala ya kuongeza juhudi na maarifa katika kufanya kazi za maendeleo hatimaye kujipatia kipato, ambacho kitawasaidia wao na familia zao.

“Waislamu kama ilivyo ni dini ya amani na wote kwa ujumla, tunapenda amani kwani pasipokuwa na amani nchini watu hawataweza kwenda kufanya kazi na hata kwenda kwenye nyumba za ibada kumuabudu Mwenyezi Mungu, hivyo tunatakiwa tusiwasikilize watu wachache ambao hawaitakii mema nchi yetu,” alisema Chamwenyewe.

Alisema kuwa hata katika kitabu kitukufu cha Koran, Mwenyezi Mungu amewaamrisha Waislamu kufanya kazi na kuishi kwa amani na watu wengine wasiokuwa Waislamu, hivyo aliwataka kutokwenda kinyume na maagizo hayo ya Mwenyezi Mungu, ambaye amewaumba.

“Tusiwe kila siku tunalalamika kuwa Waislamu tunaonewa katika maeneo mbalimbali, wakati wenyewe hatufanyi bidii katika kusoma na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa,” alisema.

Chamwenyewe aliwatahadharisha kuwa akitokea mtu anawaambia wakae msikitini kutwa nzima bila kufanya kazi, wakitegemea Mwenyezi Mungu atawashushia fedha hapo walipo, jambo hilo siyo kweli, bali watakuwa wanajidangaya, kwani kufanya ibada inatakiwa kuendane na kufanya kazi, ndipo watapata mafanikio.

Siku za hivi karibuni kumekuwa na hofu miongoni mwa jamii kuhusu hatua ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutangaza operesheni ya kuzuia Udikteta Tanzania (UKUTA), ambayo itakwenda sambamba na maandamano nchi nzima Septemba Mosi mwaka huu. Hata hivyo, maandamano hayo yameshapigwa marufuku na Jeshi la Polisi.

No comments

Theme images by andynwt. Powered by Blogger.