Ads

Mmmh! JPM - Kuna Viongozi Wastaafu Wanawashwawashwa..Kila Siku Wao Ni Kukosoa Tu...!!!


Rais John Magufuli jana alionekana kukerwa na baadhi ya viongozi wastaafu wasio wa kada ya sheria ambao wamekuwa wakikosoa uendeshaji hadharani.


Akizunguza katika hafla ya kumwapisha Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Juma Ikulu jijini Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alisema majaji wakuu wastaafu wote ni waadilifu.

"Huwezi kumsikia Jaji (Mohamed Othman) Chande anazungumza chochote, huwezi kumsikia Jaji Mstaafu (Barnabas) Samata anazungumza chochote, huwezi kumsikia Jaji Augustino (Ramadhani) au (Jaji Mstaafu Damian) Lubuva wakizungumza chochote," Rais Magufuli alisema.

"Ukiangalia (ukilinganisha) na wastaafu wengine wa maeneo mengine... hawachoki kusema. wana washwawashwa."

Aidha, wakati Watanzania 465 wakisubiri kunyongwa katika magereza mbalimbali nchini, Rais Magufuli alisema hayupo tayari kutia sahihi utekelezaji wa hukumu ya kifo dhidi yao.

Alisema anatambua ugumu wa kutekeleza adhabu hiyo, hivyo akaitaka mahakama kutompelekea orodha ya waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa.

"Kazi ya ujaji mkuu ni kazi ngumu, mojawapo ni kuhukumu kunyonga, kama ambavyo mmekuwa mkifanya.

Mnapoleta kwetu kwa wanasiasa tunaogopa kuidhinisha kunyonga," alisema na kueleza zaidi: "Na ninaambiwa wapo wengi tu walioidhinishwa kunyongwa, lakini naomba hiyo orodha wala msiniletee kwa sababu ninajua ugumu wake ulivyo."

Ripoti ya Tume za Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyotolewa Mei 2015, ilibainishwa kuwa kuna Watanzania 465 wanaosubiri kunyongwa katika magereza mbalimbali nchini.

Pia Ripoti ya Mpango wa Kujitathmini kuhusu Haki na Utekelezaji wa Haki za Binadamu (UPR), unaotekelezwa kwa mara ya pili nchini, inaonyesha kuwa kuna wafungwa 465 wanaosubiri adhabu ya kifo, kati ya hao wanaume ni 445 na wanawake ni 20.

KAZI NI NGUMU

Akizungumza mbele ya wageni waliofika kushuhudia kiapo hicho, Rais Magufuli alisema kazi ya kumteua au kumchagua Jaji Mkuu ni ngumu, akieleza kuwa kabla ya uteuzi kama huo ni lazima kujua historia ya mhusika pamoja na tabia yake.

"Ninafahamu kazi ya kumteua au kumchagua Jaji Mkuu ni ngumu. Ni kama ilivyo ngumu kwa majaji wanapohukumu,” alisema.

"Ni lazima ujue historia, tabia ya yule unayemhukumu, na je, ukishamhukumu atafanya nini? Na mimi hivyo hivyo, 'nimeutaste' (nimeuonja) ujaji kidogo wakati nikimteua Jaji Mkuu.”

Rais Magufuli alisema alichukua muda kujiridhisha na utendaji wa Jaji Mkuu Prof. Juma kwa kutumia kipengele ambacho kilimruhusu kumteua Kaimu Jaji mkuu. Prof Juma aliteuliwa kuwa Kaimu Jaji Mkuu Januari 17.

"Na ndiyo maana nilitumia ibara ya 118 kifungu kidogo cha nne. Nilifanya hivyo siyo kwa maana majaji walikuwa hawafai, majaji wote ni wazuri," alisema.

Kifungu hicho kinasema pale ambapo ofisi ya Jaji Mkuu itakuwa wazi, na Rais akionelea inafaa kumteua Jaji Mkuu, anaweza kumtea Kaimu Jaji Mkuu ambaye atatekeleza majukumu ya Jaji Mkuu mpaka pale Jaji Mkuu atakapoteuliwa.

"Sikutaka kumteua Jaji, baada ya mwaka mmoja niteue tena Jaji, au baada ya miaka miwili awe amestaafu niteue mwingine.

"Nilitaka nikiteua jaji akae hata miaka 10 awe anatujaji wote tutakaokuwapo." Alisema pia alitaka kuteua Jaji Mkuu ambaye ataendana na dhamira yake ya kupambana na rushwa.

Alisema wakati anafanya uteuzi huo, walikuwapo majaji wengi waliostahili nafasi hiyo, lakini majaji wengi wamebakiza mwaka mmoja hadi mitatu kustaafu.

KAZI NYEPESI

Awali akizungumza baada ya kuapa, Jaji Mkuu Prof. Juma alisema wakati akiwa Kaimu Jaji Mkuu alifanya kazi zote anazopaswa kufanya Jaji Mkuu na hakupata shida yoyote.

“Kazi yangu sasa itakuwa nyepesi kwa sababu ya wale walionitangulia waliweka misingi mizuri. Kazi kubwa ni kuweka misingi ya haki," alisema.

Alisema kazi nyingine ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na imani na mahakama ambayo alisema itajengwa kwa kuepuka vitendo vya rushwa na ucheleweshwaji wa mashauri.

Jaji Mkuu huyo alisema kwa sasa kunahitajika ujenzi wa mahakama za mwanzo 77 katika ngazi ya wilaya, akifafanua kuwa kati ya wilaya 139 zilizopo, zenye mahakama za mwanzo ni 113 tu.

Alisema changamoto nyingine ni upungufu wa majengo, hata ambayo yapo ni chakavu huku akibainisha kuwa katika ngazi za Mahakama Kuu, kati ya mikoa 26, mikoa 12 haina majengo ya Mahakama Kuu.

"Majengo mengi ya mahakama ni mabovu, lakini tuko mbioni kujenga Mahakama Kuu za kisasa katika mikoa ya Kigoma, Morogoro, Mara, Singiga, Dodoma na Mwanza," alisema Prof. Juma.

ORODHA YA MAJAJI WAKUU TANGU UHURU:

Raph Windham - 1960-1965

Philip Georges - 1965-1971

Augostine Said - 1971-1977

Francis Nyalali - 1977-2000

Barnabas Samatta - 2000-2007

Agustino Ramadhani - 2007-2010

Mohammed Othman Chande - 2010-2017

Prof. Ibrahim Juma

No comments

Theme images by andynwt. Powered by Blogger.