JPM Afunguka Sababu Za Kuteua Kaimu Jaji Mkuu..Adai Hakulazimishwa Na Mtu Kufanya Hivyo..!!!
Rais John Magufuli amefafanua uamuzi wake wa kukaimisha nafasi ya Jaji Mkuu wa Tanzania kwa Jaji Profesa Ibrahim Juma miezi tisa iliyopita, jambo ambalo lilikosolewa na wanasiasa na wachambuzi mbalimbali nchini.
Profesa Juma alikaimu nafasi hiyo tangu Januari 18, baada ya aliyekuwa Jaji Mkuu, Othman Chande kustaafu. Juzi Juma alithibitishwa rasmi na Rais Magufuli kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.
Jaji Mkuu huyo anakuwa wa nane katika historia ya Tanzania kabla na baada ya uhuru. Majaji wakuu waliomtangulia ni Sir Raph Windhem (1960-1965), Philip Georges (1965 - 1971) na Augustine Said (1971 - 1977). Wengine ni Francis Nyalali (1977 -2000), Barnabas Samatta (2000 - 2007), Augustino Ramadhan (2007 - 2010) na Othman Chande (2010 - 2017).
Akizungumza jana baada ya kumwapisha Profesa Juma, Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema alimteua kukaimu nafasi hiyo kwa sababu ilikuwa ni muda mfupi kwake tangu aingie madarakani hivyo alitaka kujiridhisha.
Alisema ilibidi atafute mtu wa kukaimu nafasi hiyo kwa sababu alikuwa hawafahamu majaji wengi na alitaka kupata mtu ambaye atakuwa Jaji Mkuu katika kipindi chake chote na siyo kuteua jaji mkuu mwingine baada ya miaka miwili. “Lengo langu lilikuwa ni kumpata jaji mkuu ambaye atakaa muda mrefu, mpaka pale Mungu atakapomchukua. Nataka akae miaka saba au kumi, siyo nateua mwaka huu baada ya miaka miwili tena nateua mwingine.”
“Majaji wote ni wazuri, wengine wako hapa…lakini wengi wao wamebakiza muda mfupi wa kustaafu. Mimi nilikuwa nataka mtu atakayedumu kwa muda mrefu, kwa hiyo nilikuwa na vigezo vyangu vingine,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisisitiza kuwa alifanya uamuzi huo kwa kuzingatia Ibara ya 118 (4) ya Katiba ambayo inasema;
“118 (4) Iwapo itatokea kwamba:- (a) Kiti cha Jaji Mkuu kitakuwa wazi; au (b) Jaji Mkuu hayupo Tanzania; au (c) Jaji Mkuu atashindwa kutekeleza kazi yake kwa sababu yoyote na Rais akiona kuwa kwa muda wa tukio lolote kati ya hayo matatu inafaa kumteua Kaimu Jaji Mkuu, basi Rais aweza kumteua Kaimu Jaji Mkuu kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kustahili kuteuliwa kuwa Majaji wa Mhakama ya Rufani, na huyo Kaimu Jaji Mkuu atatekeleza kazi za Jaji Mkuu mpaka atakapoteuliwa Jaji Mkuu au mpaka Jaji Mkuu mwingine ambaye alikuwa hayupo Tanzania au alikuwa hamudu kazi zake atakaporejea kazini.”
Mkuu huyo wa nchi alisema changamoto ni nyingi lakini Serikali anayoiongoza inazitambua changamoto zote zinazoikabili Mahakama nchini na kwamba tayari wameanza kuzishughulikia changamoto hizo.
“Hongera sana Jaji Mkuu, Juma. Ni Mungu ndiyo amekuchagua, kwa hiyo ukafanye kazi kwa Watanzania. Nilipokuteua wewe sikuwa na shinikizo la mtu yoyote, palikuwa na sample kubwa tu lakini nilikuwa na vigezo vyangu,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alimuomba Profesa Juma kwenda kuzifanyia kazi kesi za rushwa ili Serikali iweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Alisema wakati mwingine bajeti inakuwa ndogo kwa sababu fedha za Serikali zinapotea kwa rushwa.
“Kazi ya ujaji mkuu ni ngumu utahukumu kunyonga na nawaambia wapo wengine ambao wameshahukumiwa kunyongwa, naomba hii orodha msiniletee najua ugumu wa kazi hii,” alisema Rais Magufuli.
Akizungumzia kukaimisha ujaji mkuu, Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi alisema siyo mara ya kwanza kwa nafasi ya Jaji Mkuu kukaimiwa, jambo hilo limefanyika pia kwenye nchi mbalimbali za Jumuiya ya Madola.
Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zambia, Rais wa nchi hiyo alimteua Lombe Chibesakunda kukaimu nafasi ya Jaji Mkuu kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2012 mpaka 2015, baada ya hapo hakumthibitisha badala yake akamteua Irene Mbambilima kuwa Jaji Mkuu wa Zambia.
Jaji Mkuu Profesa Juma alisema wakati anakabidhiwa ofisi na Jaji Mkuu alikabidhiwa pia mipango kazi ya Mahakama ikiwamo kata 4,000 ambazo zinahitaji kuwa na mahakama za mwanzo.
Kuhusu kuingiliana kwa mihimili mitatu ya Serikali, Jaji Mkuu alisema mihimili hiyo ya Mahakama, Bunge na Serikali haina mgongano wowote kwa sababu maudhui ya Katiba yanaelekeza mihimili hiyo kuwatumikia wananchi na ndiyo inayounda Serikali moja.
Alisema Mahakama itahakikisha inafanya kazi kwa karibu na mihimili mingine ili kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati na kwa uwazi.
No comments