Ads

Mambo Bado, Simba Mtafurahi Sana..




MSHAMBULIAJI wa Simba, John Bocco, amesema mashabiki wa timu hiyo watafurahi zaidi msimu huu kutokana na kazi watakayoifanya uwanjani kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.


Bocco aliyazungumza hayo muda mfupi baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya Mwadui FC iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam huku nyota huyo akifunga bao moja wakati Simba ikishinda 3-0.

Bocco, alisema bao alilolifunga kwenye mchezo huo, limefungua akaunti yake ya mabao katika timu hiyo.

"Watu wametubeza sana, lakini mimi nasema tuna timu bora na mashabiki wetu watafurahi sana," alisema Bocco.

Alisema pamoja na kuitwa 'Muhenga' anaamini bado anauwezo mkubwa na atahakikisha anaendelea kufunga ili kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri.

"Sisi tutawajibu wapinzani wetu kwa vitendo, na vitendo hivyo wataviona uwanjani, wanatuambia tumezeeka, lakini tutawaonyesha," aliongeza kusema Bocco.

Bocco juzi alifunga bao lake la kwanza kwenye ligi akiwa na Simba kwenye mchezo huo wakati mabao mengine mawili yakifungwa na mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi.

Mabao hayo mawili ya Okwi yamemfanya kufumania nyavu mara sita kwenye michezo miwili aliyoichezea Simba msimu huu.

No comments

Theme images by andynwt. Powered by Blogger.