Simba ya Omog na pointi 7 ni afadhali ya msimu uliopita…
Uliona goli ambalo Vicent Angban alilofungwa na Wazir Junior katika game ya Simba SC 0-1 Toto African msimu uliopita? Uliona goli la Omari Mponda alilomfunga golikipa huyo raia wa Ivory Coast katika mechi ya kufungua msimu huu, Simba 3-1 Ndanda FC? Umeona namna Abdulrahiman Musa alivyomchungulia kipa huyo wa Simba na kufunga goli la umbali kiasi katika game ya Simba 2-1 Ruvu Shooting?
Simba tayari wamefanikiwa kukusanya alama 7 katika michezo mitatu waliyokwisha cheza msimu huu! Ni kiwango pungufu ukilinganisha na namna walivyoanza msimu uliopita mwaka mmoja nyuma. Ushindi dhidi ya Ndanda ulikuwa ni wa ‘wasiwasi mwingi,’ na suluhu-tasa mbele ya JKT Ruvu ukaanza kuleta mashaka kama kweli timu hiyo inaweza kumaliza ukame wa miaka minne bila taji la VPL.
Nilishasema kwamba timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi inahitaji vipaji bora zaidi ili kushinda taji hilo waliloshinda kwa mara ya mwisho msimu wa 2011/12.
Ukilinganisha na wapinzani wao wa sasa katika mbio za ubingwa, timu za Yanga SC iliyoshinda mataji matatu katika misimu minne iliyopita ( 2012/13, 2014/15, na 2015/16) na Azam iliyoshinda taji lake pekee 2013/14 (pasipo kupoteza mechi,) utaona Simba haina ubavu wa kushinda taji hilo.
Matatizo ya kiutawala yaliinyima timu hiyo nafasi ya ubingwa msimu uliopita, na badala ya kuanzia pale walipoishia msimu uliopita wameanza upya kabisa na matokeo yake yanaanza kujidhihirisha mapema.
Walipata ushindi kwa mara ya kwanza baada ya kupita kwa miaka mitatu katika uwanja wa Mkwakwani, Septemba 2015. Ilikuwa ni dhidi ya timu dhaifu na ambayo ilicheza zaidi ya michezo 8 pasipo kufunga goli-African Sports ambayo ilikuwa ikicheza Ligi kuu kwa mara ya kwanza baada ya kusubiri kwa miaka 23.
Ushindi huo wa 2-0 uliambatana na utambulisho wa mshambulizi mpya (wakati huo,) Mganda, Hamis Kiiza. Wakaifunga kwa mara ya kwanza JKT Mgambo katika uwanja wa Mkwakwani baada ya kushindwa kuifunga timu hiyo katika misimu mitatu ya nyuma.
Wakaondoka, Tanga wakiwa na alama 6, na kurejea Dar es Salaam kucheza na timu ‘inayowasumbua’ sana, Kagera Sugar. Kiiza akafunga ‘Hat-trick’ na kufikisha goli tano katika game tatu. Msimu huu, mechi zote 3 wamecheza Dar na watacheza pia na Mtibwa Sugar wikendi hii, kisha Azam na Yanga. Nini kitatokea?
Ni kuanza kupoteza mwelekeo wa kikosi cha kocha Mcameroon, Joseph Omog na msaidizi wake, Mganda, Jackson Mayanja. Itazame, Simba inavyocheza, wapo ‘legelege,’ hawana ubunifu katikati ya uwanja, huku benchi la ufundi likishindwa kujua ni yupi anafaa kuwa straika namba moja kati ya Mrundi, Laudit, Mavugo na Ibrahim Ajib.
Omog hajui ni kwanini timu yake inashambulia vizuri akiwepo, Mudhamir Yassin katikati ya uwanja na inapwaya asipokuwapo. Mayanja hamwambii chochote, golikipa Vicent kuhusu makosa yake ya kutoka hovyo na kuwa mbali na goli lake.
Hernandez anawasoma, Hans atawaadhibu, Salum Mayanja anatamani muendelee kucheza hivyo hata ykatika game yenu ya Jumapili ijayo.
Mimi si kocha, ila katika ‘lugha ya miili’ ya wachezaji wengi wa nafasi ya ulinzi katika VPL wanamuhofu sana, Ajib kuliko mchezaji mwingine yeyote yule.
Lakini nilishangazwa na Omog pale alipoamua kumuweka benchi kijana huyo katika game dhidi ya JKT Ruvu na kumuanzisha, Muivory Coast, Federick Blagnon sambamba na Mavugo kisa tu mchezaji huyo wa kulipwa alifunga goli la kufungua ugumu dhidi ya Ndanda akitokea benchi katika game ya ufunguzi.
Nilishangazwa zaidi na mashabiki wa timu hiyo ambao wamekuwa wakimshutumu Ajib na kumuita ‘mbinafsi.’ Kwa mchezaji wa nafasi ya ushambuliaji, ili kuwa bora na makini anapaswa kupiga mashuti mengi zaidi golini kwa kipa wa timu pinzani.
Bila kushuti golini hamtapa goli, na kama uwezo wenu ni mdogo kiufungaji hamuwezi kushinda mechi. Ajib ni kijana mdogo na bahati nzuri kila mechi amekuwa katika kiwango kipya kinachopanda. Huyu ndiye anapaswa kuwa mshambuliaji namba moja na ili Simba ipate magoli inapaswa imtazame Ajib katika mifumo yote ya kiuchezaji. Vinginevyo hakuna magoli.
Mavugo vs Ajib, kwa kocha yeyote chaguo la kwanza kiufungaji ni Ajib. Anatisha sana kwa walinzi wa timu pinzani, anakasi, mjanja wa kutafuta mikwaju ya penalti, ana penda kushuti golini, na amekuwa na mtazamo wa kufunga tu kila anapokuwa uwanjani. Wote, yeye na Mavugo wamefunga magoli mawili mawili katika game 3 za mwanzo wa msimu.
Wakati, Mzimbabwe, Justice Majabvi alivyotangaza kuachana na timu hiyo kwa sababu za kifamilia, niliamini Simba ‘itasafa’ kumpata kiungo makini wa ulinzi ambaye ni kiongozi shupavu kwa wenzake. Lakini naona wamempata haraka sana, lakini Omog ni kama ilivyo kwa wachezaji wake Mwinyi Kazimoto na nahodha, Jonas Mkude ni ‘vipima joto.’
Leo vipo juu lakini kesho havipo juu, hali ya hewa na mabadililo yake yanapelekea tofauti hiyo. Uliona Simba ilivyocheza dhidi ya Shooting baada ya kuingia kwa Mudhamir? Uliona nini? Nitawaambia siku nyingine, ila katika kikosi cha kocha makini, Mudhamir hakai benchi.
Bado hakuna beki makini zaidi ya Juuko Murishid katika safu ya kati. Baada ya mechi 3 zijazo mtamuona yule ‘kibabu’ wenu, Method Mwanjali alivyo dhaifu. Vicent endelea kutoka golini, Omog endelea kubahatisha katika upangaji wa timu, mashabiki endeleeni kumuita, Ajib ‘mchoyo!.’ Msimu uliopita na sasa takwimu zimeanza kuwahukumu.
Shafii dauda
No comments