Messi ana mkataba wa maisha na Barca – Rais Barcelona....
Rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu ameviambia vyombo vya habari kwamba staa wao, Lionel Messi ana mkataba wa milele na klabu yao wakati huu wakijiandaa kufanya majadiliano ya mkabata mpya katika miezi ijayo.
Messi, 29, ana mkataba ambao utafikia ukomo June 2018. Pamoja na hayo, katika majira haya ya joto, staa huyo wa Argentina alihusishwa na mpango wa kuungana tena na kocha wake wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola, katika klabu ya Manchester City pia kurudi katika klabu yake ya utotoni, Newell’s Old Boys baada ya World Cup 2018, kitu ambacho Messi mwenyewe alisema angependa iwe hivyo.
Bartomeu amefanya mazungumzo ya kuongeza mkataba wa Messi kuwa kipaumbele hivi sasa.
“Messi ana miaka yote anayotaka kuwa nayo na Barcelona. Lionel Messi ni mchezaji bora zaidi kuwahi kuuchezea mpira wa miguu katika historia ya dunia na anaichezea timu yetu” alisema Bartomeu. “Tuna furaha sana, ni mtu muhimu sana kwa klabu, ni muhimu sana kwa mashabiki, ni muhimu sana kwa mpira wenyewe”
“Na tunaenda kuongea naye katika miezi inayokuja na yeye anajua, na anajua tayari ana mkataba wa milele. Hakuna ukomo kwake.”
“Ukomo utaamuliwa na yeye, kwa sasa ana miaka 29, ana kipaji na malengo makubwa, yupo katika umbo zuri kuendelea kung’aa kwa miaka mingi ijayo”
Bartomeu alienda mbele na kusema anategemea majadiliano yatamalizika haraka, aliongeza: “Kwa sasa, tunadhani tutalifanya hili katika miezi ijayo, na Lionel Messi ataendelea kuwepo Barcelona, kwa hakika”
Messi alirudi kuichezea timu yake ya taifa wiki iliyopita baada ya kustaafu kwa muda mfupi hiyo ikiwa ni baada ya kuumizwa na kufungwa kwa penati dhidi ya Chile katika fainali ya Copa America.
Aliisaidia timu yake katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Uruguay, japokuwa aliumia wakati mechi ikielekea kuisha hivyo hakuweza kucheza katika mechi ambayo Argentina ilitoka sare ya 2-2 na Venezuela, Jumanne. Barcelona bado hawajasema tarehe ambayo Messi atarejea.
No comments