NDANDA VS YANGA – KULINDA REKODI VS KUVUNJA REKODI......
Ligi kuu Tanzania bara itaendelea tena Jumatano ya September 7 kwa mechi tatu kuchezwa kwenye viwanja tofauti, game ya Ndanda FC vs Yanga ni miongoni mwa mechi kali inayosubiriwa kwa hamu na wadau wa soka kutokana na rekodi zilizopo kati ya timu hizi mbili tangu zimeanza kukutana kwenye ligi baada ya Ndanda kupanda daraja miaka ya hivi karibuni.
Ndanda watakuwa wenyeji wa mchezo huo utakaochezwa kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara kusini mwa Tanzania.
Inatabiriwa mechi hii kuwa ngumu kwa kila upande, ugumu unaosababishwa na matokeo ya timu hizi tangu zilipoanza kukutana. Kila timu itataka kutengeneza rekodi yake, Ndanda wakitaka kutunza rekodi ya kutopoteza mchezo dhidi ya Yanga wakiwa nyumbani wakati Yanga wao wakitaka kuvunja mwiko kwa kuifunga Ndanda kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona.
Mechi zilizopita 2016-2017
Ndanda imeshacheza mechi mbili na kupoteza mechi zote ambapo imecheza nje ya uwanja wake. Ilifungwa 3-1 dhidi ya Simba kwenye mchezo wa ufunguzi wa ligi kwenye uwanja wa taifa ilikuwa ni August 20, 2016. Ikasafiri hadi Manungu Turiani kucheza na Mtibwa Sugar pia ikachezea kichapo cha magoli 2-1 ikiwa ni siku saba baada ya kupoteza dhidi ya Simba.
Yanga yenyewe imecheza mechi moja pekee hii ni kutokana na kukabiliwa na mechi ya kimataifa, wakaukosa mchezo wa ufunguzi wa ligi kutokana na kuwa na mechi dhidi ya TP Mazembe.
Mabingwa hao wa msimu uliopita wakapata ushindi kwenye mchezo wao wa kwanza wa ligi dhi ya timu iliyopanda daraja Africans Lyon. Magoli ya Deus Kaseke, Simon Msuva na Juma Mahadh yakaipa Yanga ushindi wa magoli 3-0 kwenye uwanja wa taifa.
Tofauti ya nafasi katika msimamo wa VPL 2016-17
Baada ya michezo ya mwishoni mwa juma lililopita, Ndanda inashika nafasi ya 15 baada ya kucheza mechi mbili na kupoteza mechi zote hivyo haina pointi wakati Yanga yenyewe inakamata nafasi ya nane ikiwa na pointi tatu baada ya kucheza mchezo mmoja huku ikiwa na kiporo cha mchezo mmoja dhidi ya JKT Ruvu.
Ndanda wakiwa uwanja wa Nangwanda watakuwa hawana kingine zaidi ya kutafufuta ushinsi wao wa kwanza msimu huu wakiwa nyumbani wakati Yanga pia watakuwa wakitafuta ushindi wao wa kwanza kwenye uwanja huo dhidi ya Ndanda FC.
Magoli ya kufunga na kufungwa
Safu ya ulinzi ya Ndanda imesharuhusu magoli matano wakati washambuliaji wao wakiwa wamepachika magoli mawili katika mechi mbili walizocheza. Magoli matatu ya Yanga yamefungwa na viungo wazawa Deus Kaseke, Simon Msuva na Juma Mahadh huku washambuliaji Tambwe na Ngoma wakiwa bado hawajafunga licha ya kuanza kwenye kikosi dhidi ya Lyon, Yanga haijaruhusu goli baada ya mechi moja.
Rekodi Ndanda vs Yanga head-to-head
Yanga imefanikiwa kuifunga Ndanda mara moja katika mechi nne walizokutana kwenye ligi kuu bara. February 1, 2015 Yanga ikiwa mwenyeji ililazimishwa sare ya bila kufungana kwenye uwanja wa taifa kabla ya kuchapwa 1-0 kwenye mechi ya marudiano mjini Mtwara siku ya mwisho ya kufunga msimu wa 2014/15 ilikuwa ni May 9, 2015.
Msimu uliopita 2015/16 mchezo wa raundi ya kwanza uliochezwa January 17, Yanga iliifunga Ndanda goli 1-0 kwenye uwanja wa taifa na kuibuka na pointi tatu wakati mechi ya pili iliyotakiwa ichezwe Mtwara lakini ikahamishiwa Dar, Ndanda waliilazimisha Yanga sare ya kufunga magoli 2-2 hiyo ilikuwa ni May 15, 2015.
Tangu timu hizi zimeanza kukutana, yamefungwa magoli sita (6) huku kila timu ikiwa imefunga magoli matatu. Kila timu imepata ushindi mara moja, sare zikiwa mbili na kila timu imepoteza mara moja dhidi ya mwenzie. Katika ushindi ambao timu hizo zilipata, kila timu ilikuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani.
Telela, Chove, Makassi dhidi ya timu yao ya zamani
Salum Telela atakuwa akicheza kwa mara ya kwanza dhidi ya Yanga tangu alipomaliza mkataba wake msimu uliopita na klabu hiyo kumwachia aondoke akiwa mchezaji huru hatimaye akajiunga na Ndanda FC. Kwa upande wa Ndanda FC, mlinda mlango Jackson Chove na Kiggi Makasi waliwahi kuitumikia Yanga misimu kadhaa iliyopita.
Yanga bila nyota sita
Deogratius Munishi, Geofrey Mwashiuya, Pato Ngonyani, Haruna Niyonzima na Vicent Bosou ni wachezaji wa Yanga wataukosa mchezo huo kutokana na sababu mbalimbali.
No comments