Heka heka ya JPM zamu hii imeangukia bandarini mawaziri na vigogo wapata tabu baada ya. ...
Rais John Magufuli jana aliwahenyesha mawaziri wawili pamoja na vigogo wakubwa wanne baada ya kufanya ukaguzi wa ghafla katika Bandari ya Dar es Salaam.
Rais alifikia uamuzi huo akionekana kujua uwepo wa magari 53 aina ya Suzuki ambayo ni maalumu kwa kubebea wagonjwa na malori zaidi ya 50 ya Jeshi la Polisi ambayo yaliingizwa tangu mwaka 2015, lakini hayajatolewa bandarini.
Alienda eneo la maegesho ya magari mara baada ya hafla fupi ya kuwaaga mabaharia wa meli ya Peace Arc waliokuwa wakitoa huduma ya matibabu kwa wiki moja bandarini hapo.
Akionekana kama wakili anayewabana mashahidi wa upande mwingine, Rais aliuliza maswali kutoka kwa waziri mmoja hadi mwingine, na mtumishi mmoja wa Serikali hadi mwingine.
Maswali yake yalilenga kutaka kujua aliyeagiza magari hayo, sababu za taarifa kutotolewa kwa takriban miaka miwili, wahusika kutofuatilia magari waliyoagiziwa na vyombo vya dola kutofuatilia suala hilo, huku vigogo hao wakiwa wamekutanisha mikono mbele kuonyesha unyenyekevu.
Waliowekwa katika hali ngumu jana ni Dk Philip Mpango, ambaye ni waziri wa Fedha na Mipango, Profesa Makame Mbarawa (waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Valentino Mlowola (mkurugenzi mkuu Takukuru), Simon Siro (mkuu wa Jeshi la Polisi), George Mnyitafu (kaimu kamishna wa forodha wa Mamlaka ya Mapato) na Deusdedit Kakoko (mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari).
Wengi walionekana kupata taarifa za magari hayo wakati huo, kiasi cha kumfanya Rais aonekane kutoridhishwa na utendaji wao wa kutofuatilia vizuri kazi zao na kufanya magari mengine kukaa bandarini kwa takriban miaka kumi wakati sheria inaruhusu siku 21.
“I’m sorry jamani, haya mengine ni frustration zangu. Nisameheni sana,” alisema Rais Magufuli baada ya kueleza udhaifu wa utendaji wa vigogo hao wa kutochukua hatua.
Rais, ambaye alisema ana taarifa za magari hayo na mtu aliyeyaagiza, alitoa siku saba kwa mawaziri na wakuu hao wa taasisi wawe wamempa taarifa kamili ya suala hilo.
Kabla ya kutoa maagizo hayo, Rais Magufuli aliwahoji mawaziri na viongozi hao wa taasisi ambao kila mmoja alipewa kipaza sauti ili majibu yake yasikike.
Alianza kwa kumhoji Kakoko kuhusu uhalali wa magari hayo kukaa bandarini kwa muda mrefu na aliyeyaagiza.
Rais Magufuli: Nataka kujua haya magari ni ya nani?
Kakoko: Haya magari yameingia wakati hujaingia madarakani, ila yameingizwa na Ofisi ya Rais. Jina la aliyeyaagiza ni la Kichina au Kihindi hivi, lakini anwani ya mwingizaji ni Ofisi ya Rais ingawa na lenyewe limeandikwa vibaya vibaya na hata maneno yana utofauti. Magari yapo 50.
Rais: Kwa hiyo yameagizwa na ofisi yangu? Kuna mtu yeyote wa ofisi yangu ambaye aliagiza?
Kakoko: Hili jina si la mtu wa ofisini kwako na anuani si ya ofisi yako, bali ni lile jina la mwanzo tu.
Rais: Lakini wanasema yameagizwa na Ofisi ya Rais?
Kakoko: Ndivyo nyaraka zinavyoonyesha.
Rais: Mmeshafanya juhudi gani kama tangu mwaka 2015 Rais ameagiza magari kwa jina la Kichina na hayajachukuliwa na yamekaa hapa kwa jina la Kichina mpaka leo. Ulifanyaje? Ulimjulisha waziri? Na yeye anasema ndiyo amepata taarifa leo.
Kakoko: Utaratibu wetu baada ya siku 21 huwa unahama kwetu. Kimsingi yanakuwa yamehamia TRA.
Rais: Kamishna wa TRA yupo hapa hebu tueleze kuhusu haya magari ya Rais.
Mnyitafu: Rais ni kweli magari haya yaliingia mwaka 2015 Juni na taratibu zetu za kiforodha ilitakiwa tuyatangaze baada ya siku 21 ili yaweze kuuzwa.
Rais: Mliyatangaza?
Mnyitafu: Bado baada ya kushauriana na uongozi…
Rais: Mlishauriana na uongozi gani? Nataka jibu ndiyo maana nimewaita viongozi wote hapa.
Mnyitafu: Uongozi wa mamlaka wa wakati huo, tukashauriana, lakini sikuwepo wakati huo.
Rais: Nani ulimhusisha kwenye uongozi ule taja tu majina.
Mnyitafu: Sikuwepo.
Rais: Ulijuaje kama walishauriana wakati hukuwepo?
Mnyitafu: Nilivyouliza kwa wenzangu ambao…
Rais: Nani jina lake?
Mnyitafu: Maofisa ambao wapo bandarini.
Rais: Ulimuuliza nani, taja jina lake?
Mnyitafu: Meneja wa bandari ambaye yupo sasa hivi. Hata hivyo yeye ni mgeni anasema aliambiwa.
Rais: Nataka uwe muwazi, wewe si msomi bwana? Mimi mpaka kuja hapa nina taarifa nyingi ndiyo maana nataka uwe wazi ili nijue. Si umemuona mwenzako amesema wazi ofisi yangu ndiyo ilihusika mwaka 2015?
Mnyitafu: Sisi tunaangalia mtu wa kwanza aliyeagiza ambapo inasomeka kama imeagizwa na Ofisi ya Rais.
Rais: Ameshakuja mteja yeyote kufuata magari haya hapa?
Mnyitafu: Hajaja mteja yeyote kuchukua magari haya.
Rais: Ina maana hamjafanya upelelezi wowote kutambua kwamba haya magari ni ya nani?
Mnyitafu: Tuliamini kwamba ni ya Ofisi ya Rais.
Rais: Labda niulize swali jingine. Magari ya polisi yalikuja lini na haya pia yalikuja kipindi gani?
Mnyitafu: Yamekuja mwaka 2015 mwezi Juni.
Rais: Ndiyo maana nauliza magari ya polisi yalikuja mwezi wa sita na haya ya mtu ambaye hajulikani yamekuja Juni huyu hajayachukua? Polisi magari yenu yapo mangapi?
IGP Sirro: Yapo 55.
Rais: Sirro, haya magari 50 ambayo ni ambulance yanawahusu ninyi?
IGP Sirro: Hapana kwa kweli hatuyatambui na hatujui chochote kuhusu magari haya.
Rais: Nani mwingine anayefahamu kuhusu haya magari? Waziri pia hujui chochote.
Profesa Mbarawa: Mimi sijui. Nimepata taarifa leo asubuhi.
Rais: Kwa hiyo tangu mwaka 2015 Juni aliyekuwa mkurugenzi wa pale TPA mpaka ameondoka ndugu (Madeni) Kipande hakutoa taarifa na aliyeingia naye hakutoa taarifa na wewe waziri watu wako wa TRA waliokuwepo na walioko mpaka sasa hivi hawajaeleza kuwa kuna magari hamsini na kitu ambayo yamekaa hapo kwa miaka miwili, ambayo hayana mwenyewe, yameandikwa hapa president’s office wala hata mimi sijaulizwa. Mtu wa PCB, hebu njoo hapa wewe unafahamu kuhusu hili kwa sababu wewe ndiyo mtumiaji na mpelelezi mzuri. Unafahamu chochote kuhusu haya magari?
Mlowola: Kwa sasa sijui chochote mheshimiwa Rais. Ndiyo kwanza nimepata taarifa hii.
Rais: Na wewe ndiyo umepata taarifa hii leo kwa hiyo mtu wako wa PCB anayekaa bandarini naye hajui? Sheria za TRA zinasemaje Mheshimiwa Waziri? Gari linaweza likakaa humu hata miaka 30 mnatunza tu?
Waziri Mpango: Hapana mheshimiwa Rais. Sheria zinaweka ukomo wa muda na baada ya hapo inabidi zinadiwe.
Rais: Sasa kwa nini haya hayajanadiwa wala hayajatangazwa mnada kuanzia mwaka 2015?
Waziri Mpango: Kwa kweli kama nilivyosema sijui labda kamishna wa customs (ushuru) anisaidie kwa idhini yako.
Rais: Kamishna wa customs (ushuru) kwa nini hayajanadiwa au ulipewa rushwa kusudi usinadi ili kusudi siku tutakapokuwa tunatoa magari ya Serikali na haya yatoke?
Kamishna wa Forodha: Hapana mheshimiwa kama nilivyosema kwamba haya magari yaliandikwa ofisi ya Rais na siyo ofisi ya Rais tu kwa Serikali.
Rais: Kwa nini hukuandika barua kuuliza ofisi ya Rais, na Rais yupo.
Mnyitafu: Mheshimiwa tumeunda kikosi kazi kwa sababu ya kupitia magari haya pamoja na mengine. Mengi ambayo yapo bandarini ni matatizo kama haya
Rais: Kwa hiyo yako magari mengi yaliyoandikwa Ofisi ya Rais
Mnyitafu: Hapana, magari ambayo yamepitiliza muda wa kukaa bandarini lakini hayajauzwa.
Rais: Magari ya polisi yamebaki mangapi?
Mnyitafu: Ninayoyafahamu yapo 32 yapo 28 na mengine manne.
Rais: Wewe unayafahamu mangapi?
Kakoko: Yapo ya awamu tatu, ambayo hayajachukuliwa, yaliyochukuliwa zamani, lakini hayo ambayo wamesema wanagawiwa ya awamu tatu yapo kadri 53.
Akatoa maagizo haya
Baada ya kuhoji kwa muda mrefu, Rais Magufuli alitoa maagizo akitaka apate majibu ya magari hayo ndani ya siku saba ikiwa ni pamoja na kumjua mmiliki.
Alisema taarifa aliyonayo hawezi kuisema, bali anataka wamtajie mmiliki ili aweze kulinganisha na kujua kama wanafanya kazi pamoja naye.
“Kuna sababu magari haya yamefichwa kutoka bandarini kule kote yamekuja yakafichwa hapa na yaliagizwa pamoja na magari ya Serikali,” alisema Rais.
“Walipanga siku magari ya Serikali yakitolewa, na haya nayo yatoke na hiyo ninawapa njia. Ila nataka mfanye juhudi wapatikane hawa wote na kama wapo katika Ofisi ya Rais, muwapate kwa sababu hatuwezi kwenda kwa mchezo huu. Matapeli wanakuja na kusema huu ni mzigo wa Rais?
“Wamejua sasa hawawezi wakacheza vyovyote wamekuja wanayaficha hapa na aliyekuja akayatoa yalipokuwa akaja akayaficha hapa nina uhakika TRA na TPA mnafahamu kwa hiyo nataka majibu.”
Akifungua Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani Mei 9, 2015, waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, Mathias Chikawe alisema Serikali ilipanga kununua magari yapatayo 700 kwa ajili ya Jeshi la Polisi na kwamba huo ulikuwa ni mkakati pia wa kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu.
“Kwenye bajeti hii polisi imepata ongezeko zuri tu, hasa kwenye vifaa wametenga fedha za kutosha. Tunakusudia kwa ajili ya kujipanga kwa chaguzi kubwa mbili zijazo kununua si chini ya magari 700,” alisema Chikawe.
No comments