Mwana wa Gaddafi Saif al-Islam aachiliwa huru Libya...
Saif al-Islam Gaddafi, mwana wa pili wa aliyekuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi anadaiwa kuwa huru baada ya kuzuiliwa kwa kipindi cha miaka sita.
Kuna wasiwasi huenda hatua hiyo ikatikisa zaidi hali ya kisiasa na kiusalama nchini Libya.
Saif al-Islam anadaiwa kuachiliwa huru baada ya kupewa msamaha.
Ndiye aliyependelewa na babake kuwa mrithi wake na amekuwa akizuiliwa na kundi la wanamgambo katika mji wa Zintan kwa miaka sita.
Wanamgambo hao wa Abu Bakr al-Siddiq Battalion walisema aliachiliwa huru Ijumaa lakini bado hajaoneshwa hadharani.
Taarifa nchini Libya zinasema kwa sasa amo katika mji wa Bayda, mashariki mwa Libya, kwa jamaa zake.
Wanamgambo hao wanadaiwa kumuachilia huru baada ya ombi kutoka kwa "serikali ya muda".
Serikali hiyo - yenye makao yake mashariki mwa nchi hiyo - ilikuwa tayari imetoa msamaha kwa Saif al-Islam.
Hata hivyo, alikuwa amehukumiwa kifo na mahakama mjini Tripoli, magharibi mwa nchi hiyo bila yeye kuwepo mahakamani.
Maeneo ya magharibi yanatawaliwa na serikali inayopingana na serikali ya mashariki mwa Libya, lakini serikali hiyo ya magharibi yenye makao yake makuu Tripoli ndiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Kwa kirefu, inafahamika kama Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa.
Taarifa zilizowahi kutolewa awali kuhusu kuachiliwa kwa Saif al-Islam Gaddafi baadaye zilibainika kuwa na uongo.
Uchanganuzi wa Orla Guerin, BBC News, Tripoli
Ikithibitishwa kwamba Saif al-Islam Gaddafi ameachiliwa huru, hilo huenda likaongeza wasiwasi na kutotabirika katika siasa Libya.
Alikamatwa jangwani Novemba 2011 akijaribu kutorokea Niger, na baadaye akaoneshwa kwenye runinga akiwa bila vidole kadha.
Alionekana na mataifa ya Magharibi kama sura ya hadharani ya utawala wa Gaddafi na ndiye aliyeonekana kupendelewa na babake kuwa mrithi wake.
Ingawa anachukiwa sana na wengi - nyumbani na nje ya nchi - bado ana uungwaji mkono fulani Libya na huenda akajiingiza katika siasa humo.
Anatafutwa pia na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu, makosa anayodaiwa kuyatekeleza wakati wa juhudi zilizofeli za kujaribu kuzima maasi kabla ya babake kuondolewa madarakani na kuuawa.
Saif al-Islam, alitunukiwa shahada ya uzamifu (PhD) kwa njia yenye utata na chuo kikuu cha uchumi, London School of Economics mwaka 2008.
Alikamatwa Novemba 2011 baada ya kuwa mafichoni kwa miezi mitatu kufuatia kuondolewa madarakani kwa babake, Kanali Gaddafi.
Awali, alikuwa ametekeleza mchango muhimu katika kufufua na kujenga upya uhusiano kati ya serikali ya babake na nchi za Magharibi baada ya 2000.
Alitazamwa na mataifa hayo kama mwanamageuzi na mpenda mabadiliko katika serikali ya babake.
Lakini baada ya maasi ya mwaka 2011, alijipata akituhumiwa kuchochea ghasia na mauaji ya waandamanaji.
Miaka minne baadaye, alihukumiwa kuuawa kwa kupigwa risasi baada ya kukamilishwa kwa kesi iliyomhusisha yeye na washirika 30 wa karibu sana wa Gaddafi.
Saif al-Islam: Mrithi aliyegeuka mfungwa
- Juni 1972: Azaliwa Tripoli, Libya, mwana wa pili wa kiume wa kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi
- Februari 2011: Maasi dhdii ya utawala wa Gaddafi ryaanza
- Juni 2011: Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) yatoa kibali cha kukamatwa kwa Saif al-Islam kwa tuhuma za kutenda makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu
- Agosti 2011: Aukimbia mji mkuu baada ya Tripoli kutekwa an wapiganaji waliokuwa wanaipinga serikali; atorokea Bani Walid
- Oktoba 2011: Babake na kakake mdogo wauawa
- 19 Novemba 2011: Akamatwa na wanamgambo akitorokea Niger, kusini mwa Libya. Azuiliwa Zintan
- Julai 2015: Ahukumiwa kifo na mahakama Tripoli bila yeye kuwepo mahakamani
- Juni 2017: Aachiliwa huru baada ya msamaha uliotolewa na moja ya serikali mbili zinazoshindania kuongoza Libya
chanzo bbc swahili.
No comments