Cheick Tiote: Mchezaji wa zamani wa Newcastle afariki dunia
Kiungo wa zamani wa timu ya Newcastle United Cheick Tiote amefariki dunia akiwa an miaka 30 baada ya kuzimia wakati wa mazoezi nchini China, msemaji wa mchezaji huyo amesema.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast alikaa miaka saba Newcastle na kuwachezea mechi 138 ligini.
Alihamia klabu ya Beijing Enterprises mwezi Februari.
"Ni kwa huzuni kubwa ambapo ninathibitisha kwamba Cheick Tiote alifariki mapema leo baada ya kuzimia wakati wa mazoezi," msemaji wake alisema.
"Hatuwezi kusema zaidi kwa sasa na tunaomba kwamba familia yake iheshimiwe kipindi hiki kigumu. Tunaomba maombi yenu."
Tiote alizaliwa Ivory Coast na alikuwa kwenye kikosi kilichoshinda Kombe la Mataifa ya Afrika 2015.
Alianza uchezaji wake wa soka ya kulipwa Ubelgiji akiwa na klabu ya Anderlecht mwaka 2005 kabla ya kuhamia FC Twente ya Uholanzi ambapo alicheza mechi 86 na kushinda taji la ligi ya Eredivisie msimu wa 2009-10 chini ya meneja Steve McLaren.
Tiote, ambaye ni kiungo wa kati mkabaji, kisha alihamia Newcastle mwaka 2010 kwa £3.5m.
Mwaka 2011, alifunga bao linalokumbukwa sana alipowasaidia Newcastle United kujikwamua kutoka 4-0 chini Ligi ya Premia dhidi ya Arsenal na kutoka sare.
No comments