KUMEKUCHA CCM WAAMUA KUTUMBUA MAJIPU....
Wanachama wanaotaka kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM, sasa watalazimika kuwa wakazi wa eneo wanalotaka kuliwakilisha, sharti ambalo linaweza kuwaondoa takriban nusu ya wabunge wa sasa.
Kutokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuruhusu mtu kwenda sehemu yoyote apendayo, imekuwa rahisi kwa mtu kuishi mji kama Dar es Salaam na kugombea ubunge wa jimbo lililoko katika mkoa mwingine.
Na uhuru huo umewawezesha watu kama Augustine Mrema, ambaye ni mwenyekiti wa chama cha TLP, kuwa mbunge wa Moshi Vijijini kwa tiketi ya CCM, Temeke (NCCR-Mageuzi) na Vunjo (TLP).
Na ni kutokana na uhuru huo, wabunge wengi wa vyama tofauti, wanaishi Dar es Salaam na kuwakilisha majimbo ya maeneo ya asili yao.
Hata wafanyakazi kutoka serikalini, hasa wakuu wa mikoa na wilaya na sehemu nyingine, huchukua likizo wakati wa uteuzi wa wagombea na kwenda maeneo yao asilia au waliyokulia kuomba wapitishwe na wasipopitishwa hurejea makazini.
Lakini masharti mapya ya CCM yanazuia mwanachama kugombea ubunge, udiwani au nafasi nyingine yoyote bila ya kuwa mkazi wa eneo hilo.
“Shika maneno yangu, mwaka 2020 wagombea ubunge watakuwa ni wale ambao wanatoka kwenye maeneo husika, wanaojua na kushughulika na shida za wananchi,” alisema katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole katika mahojiano na kituo cha redio cha Times FM jana.
Alisema hatua hiyo imetokana na chama hicho kujitathmini na kujisahihisha baada ya kugundua watu wanataka viongozi wanaotoka miongoni mwao ambao wanajua kero zao na hivyo wataweza kuzishughulikia.
Polepole, ambaye alipata umaarufu wakati wa Bunge la Katiba akitaka litumie rasimu iliyotokana na maoni ya wananchi, alisema wanachama watakaokuwa wakazi wa maeneo tofauti na wanayotaka kuyaongoza, hawataruhusiwa.
Akihojiwa katika kipindi cha Maisha Mseto, Polepole alisema ili mwanaCCM awe na sifa za kugombea, ni lazima awe mkazi wa eneo husika.
Polepole, ambaye alikuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, alisema suala hilo lilikuwa sehemu ya maoni ya wananchi wakati wa mchakato wa Katiba Mpya.
Alisema msisitizo mkubwa uliopo ni cheo kimoja kwa mtu mmoja jambo linalofundisha kuwa watu wenye kiasi.
“Haya mambo ndiyo watu wanayoyataka. Rais (John) Magufuli alienda mbele zaidi kwamba utagombea nafasi ya uongozi kwenye eneo ambalo wewe ni mkazi vinginevyo, marufuku kugombea,” alisema Polepole.
“Mwaka 2020 unakuja, si mtu upo zako Times FM unapiga kazi, halafu ikifika mwishoni unaenda Ileje eti unaenda kuchukua jimbo.”
Akizungumzia uamuzi huo, katibu wa wabunge wa CCM, Jason Rweikiza alisema sharti hilo litakomesha tabia iliyojengeka kwa baadhi ya wanachama wa chama hicho kwenda kugombea ubunge maeneo ambayo hawajui yana matatizo gani.
“Unakuta wananchi wana shida ya maji, umeme na barabara anakuja mgombea kipindi cha uchaguzi na ahadi kemkem, kumbe yote ni kuwavutia wampigie kura na akishajihakikishia ushindi humumuoni tena,” alisema Rweikiza.
Rweikiza alisema hatua hiyo itasababisha watu wathamini kwao na kuelewa matatizo ya maeneo waliyotoka na uchaguzi utakuwa huru bila ya rushwa.
Suala la rushwa pia lilizungumzwa na Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), BensonBana ambaye aliusifia uamuzi huo.
“Huwezi kuwa mwakilishi ambaye muda wote uko Dar es Salaam unafanya biashara zako,” alisema gwiji huyo wa sayansi ya siasa.
“Kwa kuangalia dhana ya uwakilishi, ni lazima uwe ni mtu unayeishi kwenye eneo hilo, unajua matatizo yao, unajenga nao barabara na kushiriki shughuli nyingine.
“Hawa watu wanaishi Dar es Salaam na tena wana fedha hivyo wanapokwenda vijijini wanakuwa na uwezo wa kutumia fedha zao kufanya kampeni na mambo mengine tofauti na wale wanaotoka maeneo hayo.”
No comments