Umri wa Kustaafu Kwa Madaktari Bingwa Sasa miaka 65
Frank Mvungi- Maelezo, Dodoma.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha muswaada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali ikiwemo sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (The Public Service Act) itakayowezesha muda wa kustaafu kwa Wahadhiri waandamizi, Maprofesa na Madaktari Bingwa kuwa miaka 60 kwa hiari na lazima miaka 65.
Akizungumza wakati akiwasilisha muswaada huo Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju amesema kuwa marekebisho katika jedwali yanapendekeza kuongezwa kwa kifungu kipya cha 25A ambacho kinaainisha kuhusu umri wa kustaafu ambapo kwa sasa sheria ilivyo haina masharti hayo isipokuwa umri wa kustaafu umetajwa katika sheria zinazoanzisha mifuko ya hifadhi za jamii.
Aliongeza kuwa, uzoefu umeonyesha kuwamba Maprofesa na Wahadhiri waandamizi wa vyuo Vikuu vya Umma pamoja na madaktari Bingwa wa Binadamu wa Hospitali za Umma wamekuwa wakihitajika kuendelea kutoa huduma, utaalamu na uzoefu wao licha yakufikisha umri wa miaka 60 kwa sasa ya kustaafu na hivyo kulazimika kuajiriwa na Serikali kwa mikataba.
Hatua yakuwaajiri wataalamu hao kwa mikataba baada ya kustaafu imetajwa kuongeza gharama kubwa kwa Serikali ambapo muswaada ulipitishwa unawezesha Serikali kuokoa Kiwango kikubwa cha fedha zilizokuwa zikitumika katika kuwalipa wataalamu wao mara baada ya kustaafu ili waweze kufanya kazi kwa mikataba.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu Sayansi na Teknplojia mhe. Profesa Joyce Ndalichako alisema kuwa anaunga mkono hoja yakuongeza umri wa kustaafu kutoka miaka 60 kwa lazima hadi 65 na kutoka miaka 55 kwa hiari hadi miaka 60.
Aliongeza kuwa Serikali inayo mikakati ya makusudi yakuwaendeleza wataalamu wa kada zenye uhaba wataalamu wabobezi ili kuziba pengo lililopo.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wake wa 10 kikao cha 1 limepitisha muswaada wa marekebisho ya sheria mbalimbali nne ambazo ni Sheria ya Ufilisi, sura ya 25, Sheria ya Bajeti, sura ya 439, Sheria ya Ardhi, sura ya 113 na Sheria ya Utumishi wa Umma, sura ya 238.
No comments