Korea Kaskazini kushiriki katika michezo ya Olimpiki nchini Korea Kusini
Korea Kaskazini imesema kuwa itatuma ujumbe wake katika michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi 2018 inayotarajiwa kufanyika Korea Kusini mnamo mwezi Februari kulingana na mji wa Seoul.
Tangazo hilo lilijiri wakati ambapo mataifa hayo yalikutana kwa mazungumzo ya kihistoria baada ya zaidi ya miaka miwili.
Ujumbe huo utashirikisha wanariadha na mashabiki miongoni mwa wengine.
Korea Kusini pia ilipendekeza kukutanisha familia zilizotenganishwa na vita vya Korea wakati wa michezo hiyo ya majira ya baridi.
Swala hilo lina utata mkubwa miongoni mwa mataifa hayo mawili, na Korea Kusini imekuwa ikipendekeza familia ziendelee kukutanishwa.
Mpango huo wa kuzikutanisha familia unatarajiwa kufanyika wakati wa likizo ya mwaka mpya, ambayo hufanyika katikati ya michezo ya Pyeongchang.
Mji wa Seoul pia uliwataka wanariadha kutoka mataifa yote ya Korea kufanya gwaride la pamoja katika sherehe ya ufunguzi ya michezo ya Olimpiki.
Haijulikani ni vipi Korea Kaskazini ilijibu mapendekezo hayo.
Mara ya mwisho kwa mataifa yote mawili kufanya gwaride la pamoja chini ya bendera ya rasi ya Korea ni zaidi ya miaka 10 iliopita katika michezo ya olimpiki ya 2006.
Waziri wa muungano wa Korea Kusini , Cho Myoung-Gyon amesema mazungumzo hayo yanajikita zaidi katika masuala ya olimpiki lakini mambo mengine pia yatajadiliwa ikiwa ni pamoja na kutumia fursa hiyo kuimarisha uhusiano.
"Tunahudhuria mkutano huu ili kuzungumzia suala la Korea Kaskazini kushiriki katika mashindano ya Olimpiki ya msimu wa baridi yatayofanyika korea kusini na kuimarisha uhusiano wan chi hizi mbili.Ninaelewa kuwa matarajio ya wengi juu ya mkutano huu ,kwanza ni kuhusu mawasiliano baina ya nchi hizi mbili ambayo yalisitishwa kwa muda.Tuna lengo la kufanya mashindano haya ya Olimpiki kuwa ya hatua ya kwanza ya kuboresha Amani baina ya nchi hizi mbili hivyo hii ni hatua nzuri na hatuna haraka."Cho Myoung-Gyon aeleza.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili uliporomoka baada ya Korea Kusini kukatisha mradi wa pamoja wa kiuchumi huko eneo la kiuchumi la Kaesong Korea Kaskazini, na kufuatiwa na majaribio ya nyuklia yaliofanywa na Korea Kaskazini.
Mazungumzo ya mwisho baina ya nchi hizo mbili yalifanyika Disemba mwaka 2015 huko Korea ya Kusini.
Siku ya Jumatatu waziri wa muungano wa Korea Kusini alisema kuwa mazungumzo hayo yatajikita zaidi katika masuala ya olimpiki lakini mambo mengine pia yatajadiliwa.
''wakati tunazungumzia masuala ya uhusiano wa Korea, serikali itazungumzia pia suala la matokeo ya vita na njia za kupunguza mvutano wa kijeshi'' alisema waziri Cho Myoung-gyon ambaye ataongoza mazungumzo hayo yatakayohudhuriwa na wawakilishi watano.
Nayo Korea Kaskazini watatuma wawakilishi watano wakiongozwa na Ri Son-gwon ambaye ni mwenyekiti wa Idara ya serikali ya Korea ya Kaskazini mwenye dhamana ya masuala na Kusini.
KWANINI MKUTANO KUFANYIKA KIJIJI CHA PANMUNJOM?
Kijiji hicho hujulikana kama kijiji cha pande mbli, ambapo kila upande una miliki sehemu yake na katikati kuna jengo la umoja wa mataifa. Baada ya vita ya korea kuisha mwaka 1953 kijiji cha Panmunjom kiliamuriwa kuwa sehemu ya pande zote mbili, na maofisa wa pande wanaweza kukutana hapo.
No comments