JPM HIVI NDIVYO MAMBO YA MIPAKANI TUNAVYO YASHUGHULIKIA
Rais John Magufuli amesema nchi za Afrika Mashariki zinashirikiana kwa karibu kuondoa vikwazo vya biashara mipakani kwa kuanzisha vituo vya pamoja vya huduma.
Alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kituo cha pamoja cha huduma Mutukula mpakani mwa Tanzania na Uganda. Alifanya uzinduzi huo pamoja na Rais Yoweri Museveni wa Uganda na baadaye wawili hao walizindua ujenzi wa bomba la mafuta kwa upande wa Uganda.
Rais Magufuli alisema mwaka jana alizindua vituo kama hicho katika mpaka wa Rusumo akiwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame na kingine cha Holili/Taveta akiwa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Alisema ataendelea kushirikiana na Uganda na nchi nyingine za Afrika Mashariki ili kuhakikisha wanaondoa vikwazo vyote vya biashara na wananchi wanafanya biashara bila shida.
Rais Magufuli alisema biashara ndani ya Afrika imebaki kuwa chini kwa sababu ya matatizo mipakani.
“Ili kuondokana na hilo, nchi za Afrika Mashariki zimeanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuanzisha vituo vya pamoja vya huduma,” alisema Rais Magufuli.
Pia, alisema mizigo na abiria sasa wanachukua muda mfupi zaidi kusafiri tofauti za zamani kutokana na ukaguzi kuchukua muda mfupi.
Alisema ukaguzi wa mizigo ya abiria unachukua nusu saa mpaka saa moja ikilinganishwa na zamani ilipokuwa inachukua kati ya saa nne hadi tano.
“Zamani malori yanayobeba makontena yalikuwa yanatumia siku nzima kufanya ukaguzi na utaratibu mwingine wa uhamiaji lakini sasa wanatumia nusu saa mpaka saa moja kukamilisha utaratibu huo,” alisema Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Rais Museveni alibainisha sekta nne alizosema ndizo zinazoleta utajiri na ajira kwa wananchi. Alizitaja kuwa ni kilimo cha kisasa, viwanda, huduma na teknolojia, habari na mawasiliano (Tehama).
Alisema sekta hizo zinaweza kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa nchi za Kiafrika.
Pia, aliwataka Watanzania na Waganda wanaoishi mpakani kutowekewa vikwazo vya kuvuka mpaka kwa sababu si dhana halisi ya kuwa na mipaka.
Rais Museveni alisema mpaka hautakiwi kuingilia maisha ya watu ambao wanaishi mpakani bali uwe ni kwa ajili ya watu wengine ambao wanatoka mbali na mizigo yao.
Wakati huohuo, viongozi hao wawili walizindua ujenzi wa bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 1,445 litakalotoka Hoima, Uganda mpaka Tanga, Tanzania uliofanyika katika kijiji cha Luzinga kilichopo Uganda.
Rais Magufuli ametaka kuharakishwa kwa ujenzi wa mradi huo ili wananchi wa nchi hizo mbili waanze kunufaika na matunda ya mradi huo ifikapo mwaka 2019.
Mradi huo wa miaka mitatu utaanza kujengwa Januari 2018 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2020. Alisema hilo litawezekana kwa kuweka makandarasi wengi.
Pia, alimshauri Rais Museveni kuwapa tuzo vijana waliogundua mafuta nchini humo kwa sababu wamefanya kazi kubwa ya kihistoria ambayo itakuwa na manufaa kwa wananchi wa nchi hiyo na Afrika Mashariki kwa jumla.
No comments