Hii hapa sababu ya chadema kujitoa kwenye uchaguzi wa madiwani
CHADEMA ilitangaza kujitoa kushiriki uchaguzi wa madiwani wa kata tano katika Halmashauri ya Meru jana mchana, kwa madai kuwa ulitawaliwa na vurugu, kupigwa mapanga, kuzuiwa kwa mawakala wake vituoni na Mbunge wa Babati Mjini, Paulina Gekul, kutekwa.
Kata hizo ambazo Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimejitoa na majina ya wagombea wake kwenye mabano ni Ambureni (Dominick Mollel), Makiba (Joyce Ruto), Maroroni (Asantael Mbise), Leguruki (Daniel Mbise) na Ngobobo (Emmanuel Salewa).
Akizungumza na waandishi wa habari hapa, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema kilichofanyika Meru siyo uchaguzi bali ni vurugu na ubabe.
Alidai "watawala" wamepanga kuwatangaza washindi wanaowafahamu kwa kutumia nguvu ya Jeshi la Polisi.
Alisema vurugu hizo zilisababisha kutekwa kwa baadhi ya viongozi wao na mawakala kuondolewa kwa nguvu vituoni.
Alisema mawakala wao walitekwa, kushambuliwa na kunyimwa kuingia katika vituo vya kupigia kura.
Alisema Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Gekul, ambaye alikuwa Kata ya Leguruki Jimbo la Arumeru Mashariki alitekwa na hakuwa akijulikana alipo mpaka mchana huo.
Kazi ya kupiga kura ilianza kwa misururu ya watu wachache majira ya saa 12 asubuhi jana, lakini iliongezeka kuanzia mchana baada ya watu kutoka kwenye nyumba za ibada.
“Vyombo vya dola vimetumika, polisi wametumika kufanya hila zote na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha (Lucas Mkumbo) anajua kila kitu,” alidai.
Alidai polisi waliwasindikiza vijana wa Green Guard wa Chama Cha Mpinduzi kupiga, kuwashambulia kwa kuwakata kwa mapanga na kuwateka mawakala wa Chadema.
"Arumeru hakuna uchaguzi," alisema Mbowe. "Wamepanga kuwatangaza washindi wanaowajua wao kwa kutumia nguvu ya dola."
Aliamuru viongozi na mawakala wa chama hicho waliokubaliwa kuingia katika vituo vya uchaguzi majira ya saa 6:00 mchana kuondoka kwenye vituo hivyo.
"Tuwaachie wao waendelee na uchaguzi huu batili na kufanya wanavyotaka kuendesha chaguzi hizo," alisema Mbowe.
"Nataka kuwaambia wagombea na mawakala wetu wasiende kwenye majumuisho ya kura.
"Nimewasiliana na Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi na amesema kuwa yupo Tunduma na nimemueleza mapungufu yote yaliyojitokeza."
Akizungumzia madai ya Mbowe, Msimamizi wa Uchaguzi katika Halmashauri za Meru na Arusha Vijijini, Dk. Wilson Mhera, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo, lakini alisema kosa lilikuwa la viongozi wa vyama.
“Vyama vyote vilitakiwa kuleta majina ya mawakala wao na vituo watakavyosimamia ili wajaze fomu namba sita pamoja na kuapishwa lakini (Chadema) hawakufanya hivyo,” alisema.
Alisema mawakala hao walileta majina siku tatu kabla ya uchaguzi ambapo jana walilazimika kusambaza barua za utambulisho wa mawakala hao kwenye vituo vyote.
Aidha alisema baadhi ya mawakala wa Chadema waligoma kupokea barua za utambulisho.
Mapema kabla ya Mbowe kutangaza kuwa chama hicho kimejitoa kushiriki uchaguzi katika kata hizo, baadhi ya mawakala wa chama hicho walizuiwa kuingia kwenye vituo vya kupigia kura.
“Baadhi ya mawakala walitolewa kwenye vituo vya kupigia kura kutokana na kutokuwa na barua za utambulisho kutoka kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi,” alisema mgombea wa udiwani Kata ya Maroroni, Daniel Mbise.
Kufuatia kuzuiwa kwa mawakala hao, wananchi walipiga kura bila kuwepo kwa mawakala wa Chadema.
No comments