Ads

ZITO ADAI YUPO TAYARI KUWAJIBIKA KWA.....


Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kama Rais John Magufuli ataruhusu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Seriakali (CAG) kuchunguza mapato ya Julai na Agosti, yupo tayari kuwajibika.


Zitto amesema hayo siku moja baada ya Rais kuagiza wanaopotosha taarifa za Serikali kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Sikumbuki vizuri, Sheria ya Takwimu ya 2015, kuna kifungu kinasema mtu anayebadilisha takwimu za Serikali anaweza kufungwa miaka miwili jela. Unakuta mtu anazungumza makusanyo yameshuka, wakati anajua si kweli. Watu wa namna hii wangekuwa wanapelekwa mahakamani waka-justify (wakathibitishe),” alisema Dk Magufuli akizungumza juzi nbaada ya kutunuku vyeti kwa wajumbe wa kamati za makinikia.

Kwa muda, Zitto amekuwa akihoji ukimya wa Serikali katika kutangaza mapato hata ilipotangaza, alisema takwimu zimepikwa kabla juzi Rais hajaamua kumtolea uvivu.

Zitto amekuwa akihoji bila majibu baada ya Benki Kuu (BoT) kutotangaza mwenendo wa uchumi kwa kila mwezi kuanzia Julai mpaka Septemba kwa kilichoelezwa kuwa ni ugumu wa upatikanaji wa taarifa lakini hivi karibuni, BoT imeweka taarifa za Julai na Agosti.

Hata Mamlaka ya Mapato (TRA) nayo ilikuwa ikisuasua kutangaza makusanyo kwa kipindi hicho kabla haijabainisha makusanyo ya robo ya kwanza ya mwaka hivyo kumpa nafasi Zitto kusema hali hiyo ilitokana na kupika taarifa.

Kwa hesabu za kawaida, kama mapato yanashuka, alisema Serikali haiwezi kusaini mkataba wa kujenga reli yenye thamani ya zaidi ya Sh7 trilioni na urefu wa kilomita zaidi ya 700 wala haiwezi kununua ndege sita mpya kwa wakati mmoja.

Baada ya kauli ya Rais juzi, kupitia ukurasa wake wa Facebook Zitto aliandika: “Kama Rais anaamini mapato hayajaporomoka, aruhusu ukaguzi maalumu wa CAG kwenye makusanyo ya Julai na Agosti na ukaguzi huo uwekwe wazi. Akifanya hivyo nitawajibika.”

Kuonyesha ana uhakika na akisemacho, mbunge huyo wa Kigoma Mjini amesema taarifa kamili kuhusu ‘kupikwa’ kwa takwimu za Pato la Taifa (GDP) wataitoa mara baada ya kikao cha Kamati Kuu ya chama chake kitakachoketi Jumamosi ya wiki hii.

Tofauti na wadau wengine, Zitto hajatishwa na agizo la Rais Magufuli kwa kubainisha kwamba Sheria ya Takwimu aliyotaja Rais haizuii tafsiri ya takwimu zinazotolewa na Serikali.

“Tunatumia takwimu za Serikali kuonyesha inadanganya kwa kutokusema uhalisia wa uchumi na kuporomoka kwa mapato,” alisema.

Alitoa mfano kwamba, Rais anaposema Serikali inatekeleza miradi mikubwa kwa kutumia ongezeko la kodi anakuwa anadanganya wananchi na anafanya hivyo akijua anachofanya.

Vilevile, alifafanua kuwa Rais anajua deni la taifa limeongezeka kwa Sh6.5 trilioni katika miaka yake miwili na anajua Serikali inatumia fedha za mashirika ya umma zilizopo Benki Kuu bila kufuata sheria kulipia baadhi ya miradi yake.

Akitambua taarifa za TRA zinazoonyesha makusanyo ya Julai yaliyokuwa Sh1.1 trilioni, Agosti Sh1.2 trilioni na Septemba Sh1.3 trilioni, Zitto alisisitiza kuwa kodi inayokusanywa na TRA inaweza kulipa mishahara na kuhudumia deni la Taifa tu.

No comments

Theme images by andynwt. Powered by Blogger.