Ads

WAZIRI AMTUMBUA JIPU KIGOGO WA TANESCO


WAZIRI wa Nishati, Merdad Kalemani, ameagiza kuondolewa kazini kwa meneja wa kituo cha kuzalisha umeme cha Kidatu kwa tuhuma za uzembe uliopelekea kukatika kwa umeme kwenye gridi ya taifa juzi.


Umeme ulikatika katika gridi ya taifa saa 12:30 jioni juzi na kupelekea sehemu kubwa ya nchi kuwa gizani, kabla ya hitilafu hiyo kurekebishwa usiku lakini ukakatika tena saa 12:03 jana asubuhi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, Waziri Kalemani alisema chanzo cha kukatika umeme juzi ni hitilafu kwenye waya wa kupelekea umeme kwenye geti la kufungulia maji katika bwawa la Kidatu linalozalisha umeme wa kiasi cha megawati 204.

Alisema hitilafu hiyo ilisababisha mtambo wa Kidatu pamoja na mitambo mingine ya kuzalisha umeme katika sehemu mbalimbali nchini kutoka kwenye gridi ya taifa na hivyo kusababisha mikoa iliyounganishwa kwenye mfumo huo kukosa umeme.

Na licha ya waya kukatika, Meneja wa Kituo hakutoa taarifa mapema, alisema.

Akielezea hatua ambazo zimechukuliwa kutokana na tatizo hilo lililojitokeza, Waziri Kalemani alisema "Huyu Wilfred (Meneja wa Kituo) nimemwelekeza mkuu wake amwondoe leo (jana) katika kituo ili hali hii isiendelee tena".

"Tunataka kuwa na wafanyakazi wenye weledi."

Mbali na kuagiza kuondolewa kwa mkuu wa kituo, Waziri Kalemani pia amemuweka kikaangoni Naibu Mkurugenzi wa Tanesco, Abdallah Ikwasa kwa kumpa masaa matatu ajieleze kwa nini umeme ulikatika kwa muda mrefu.

Kadhalika, Waziri huyo alimpa siku tatu Meneja Mdhibiti wa Shirika hilo naye ajieleze kwa nini alishin dwa kutambua sababu za kukatika kwa umeme ili zizuiliwe mapema.

Waziri Kalemani alionyeshwa kukerwa na hali hiyo baada ya kufanya ziara ya kutembelea mitambo ya umeme na mifumo ya umeme ili kukagua tatizo lililoipata gridi ya taifa na kusababisha kukatika kwa umeme karibu mikoa yote nchini, likiwamo Jiji la Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, Waziri huyo alikagua kituo cha udhibiti wa mifumo ya umeme kilichopo Ubungo na mitambo ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi I (MW 150).

Waziri huyo alisema haiwezekani nchi ikaingia gizani saa 10 hivyo alimtaka Ikwasa amuondoe katika kituo Meneja wa Kidatu kutokana na uzembe huo wa kukatika umeme.

Taarifa iliyotolewa jana Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, iliwaomba radhi wananchi kutokana na tatizo la umeme la siku mbili kuanzia juzi.

No comments

Theme images by andynwt. Powered by Blogger.