KIMEWAKA TENA UFISADI WANGUNDULIKA KWENYE UNUNUZI WA MAGARI YA WASHAWAHSA KIPINDI CHA...
JESHI la Polisi limeingia katika kashfa nyingine kutokana na kuibuka utata wa mkataba wa ununuzi wa magari 770 ya maji ya kuwasha, maarufu kama washawasha huku viongozi wake wakitoa majibu yasiyoridhisha mbele ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
Wakati mambo yakiwa hivyo, PAC imesema inakusudia kuwaita maofisa waliohusika kuingia katika kashfa hiyo huku baadhi ya wajumbe wa kamati wakimtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, kuachia ngazi.
Utata huo uliibuka katika kikao cha kamati hiyo ilipokuwa ikiwahoji viongozi wa Jeshi la Polisi na wizara kutokana na hoja za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika fungu la 28 la jeshi hilo.
Mbunge wa Kilindi, Omary Kigua, alisema magari 770 ya Jeshi la Polisi yalinunuliwa bila mkataba na malipo yake ni ya Dola za Marekani milioni 65 (zaidi ya Sh. bilioni 130).
“Kunaonekana kulikuwa na mkopo benki ya Exim sasa hapa kwa nini Jeshi la Polisi lilinunua bila mkataba? Je, ni magari yapi yaliagizwa na hawa watu wa Exim walisema riba ya mkopo huu ni Sh. ngapi?’ alihoji.
Naye Mbunge wa Magomeni, Jamal Kassim Ali alihoji mchakato mzima ulivyokuwa na ni lini mkataba uliingiwa akisema: Je, taratibu za ununuzi zilifuatwa kwa huu mchakato wote hadi mkajiridhisha na kufunga nao mkataba? Nataka kujua kama taratibu hizi zilifuatwa”.
Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka, alisema katika magari hayo 770 yalipokewa 181 bila uwapo wa mkataba wowote.
“Ukiangalia inaonekana kuwa yalinunuliwa nchini India kwa fedha ya mkopo kutoka India na viwanda vya India, hapo katikati kulikuwa na nini kwenye magari 770 yaletwe 181 tu bila mkataba bila nini?” alihoji Kaboyoka.
Alisema mchakato huo unaacha maswali ambayo hayajibiki, hivyo kamati itaangalia namna ya kulishauri Bunge hatua za kuchukua kuhusu waliohusika na ununuzi wa magari hayo.
Katibu Mkuu ajibu
Akijibu hoja hizo, Meja Jenerali Rwegasira alisema mchakato wa kununua magari hayo ulianza mwaka 2013 na kuna mkataba wa awali uliotiwa saini mwaka huo lakini kwa maelezo aliyopewa wakati anafuatilia mwaka 2016 aliambiwa kuwa mkataba haukutekelezwa.
“Kutokana na kumaliza muda wake bila kutekelezwa sijui kilichotokea lakini mkataba ulisainiwa baina ya Hazina na benki ya Exim.
Wakati niko ofisini nililetewa mkataba kuutia saini ili kazi iendelee ingawa magari yalishaletwa. Nilipoletewa mkataba kwa ajili ya kuusaini na Mwanasheria wa Serikali alishaupitia akasema hauna tatizo nikakumbuka mbona tulishalipa Dola za Marekani milioni 10 na magari 181 yalishaletwa iweje mkataba usionyeshe kuwa walishalipwa,” alisema Rwegasira.
Kutokana na hilo, alisema alimshauri Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwamba mkataba uliletwa ule ule uliokuwapo wa mwaka 2013 ambao ulikuwa hauonyeshi kama tayari kuna fedha imelipwa.
Alibainisha kuwa mkataba wa ununuzi ulikuwa Dola za Marekani milioni 29 na kati ya hizo, Dola milioni 10 zilishalipwa.
Rwegasira alisema baada ya mwanasheria kupitia mkataba ilionyesha kuwa wamelipwa fedha na ili huduma iendelee wakatia saini mkataba wa nyongeza wa Februari, mwaka huu, ambao ulionyesha kuna malipo yamefanyika.
“Baadaye walileta hati ya madai ya malipo pili, tukamshauri Katibu Mkuu Hazina tuupitie upya mkataba huu na tukaunda timu ya watu watatu mwezi uliopita kutoka Hazina, mimi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kupitia upya kujua aina ya magari na riba yake,” alisema Katibu Mkuu huyo.
Amtaka ajiuzulu
Kutokana na kuwapo utata huo na madudu mengine katika Wizara, Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, alimshauri Jenerali Rwegasira kuomba aondolewe kwenye nafasi hiyo kwa kuwa wizara imekumbwa na ubadhirifu wa mabilioni ya fedha za umma, uchafu ambao utamharibia sifa aliyoijenga kwa miaka mingi.
Alizitaja taasisi hizo ambazo zimeonekana kuwa na ubadhirifu wa mabilioni ya fedha kuwa ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Jeshi la Polisi na Idara ya Uhamiaji.
Alisema Rwegasira amefanya kazi kubwa kwenye nchi na ni kazi ya kutukuka, hivyo ni ni vyema kukabidhi kazi yake kwa Rais kama watu wa taasisi hizo wasipojirekebisha.
Naye, Mbunge wa Iramba Mashariki (CCM), Allan Kiula, alisema Katibu Mkuu huyo amefanya kazi nzuri iliyotukuka lakini kuna mambo ambayo hayaendi vizuri yanayofanywa na watu wa kada na kwamba si yeye anayesababisha.
Kiula alisema bado kwenye Wizara hiyo kuna watu ambao sio waaminifu na hamsaidii Katibu Mkuu wala watu walio juu yao.
Mishahara ewa mil. 757/-
Mbunge wa Viti Maalum, Amina Iddi Mbarouk, alisema Jeshi la Polisi lina madudu mengi na kwamba kuna mishahara ya Sh. milioni 757 imelipwa kwa wafanyakazi hewa na walipokwenda wakaguzi walikubali kuwa ni kweli watafuatilia na kuhakikisha fedha zinarejeshwa.
“Sasa ni miezi sita tangu makubaliano ya kurejesha fedha hizi, mpaka sasa kiasi gani kimerejeshwa na hatua gani zimechukuliwa kwa wahusika?” alihoji.
Akijibu maswali hayo, Kamishna wa Utawala na Fedha wa Polisi, Albert Nyamhanga, alisema kilichosababisha kuwapo na malipo hayo hewa ni kutokuwa na mamlaka ya kufuta mtu ambaye ameshakosa sifa za kuwa kwenye utumishi lakini kwa sasa suala hilo halitajitokeza tena kwa kuwa wamepewa ‘payroll point’.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa PAC, Kaboyoka, alisema majibu yaliyotolewa kwenye hoja za ukaguzi wa fungu hilo ni hafifu.
“Fedha inayozungumziwa ni mabilioni yaliyotumika vibaya kwa uzembe na inaonyesha Jeshi la Polisi kumekuwa na uzembe wa hali ya juu sana. Kuna watu wamejiwekea wigo na chini wanajua wanafanya nini na huku juu hamna muda wa kuangalia chini.
“Kamati itachukua uamuzi mgumu dhidi ya wote waliohusika kwenye mikataba ya nyuma ikiwamo kuitwa mbele ya kamati kwa sababu walijua wanachofanya,” alisema.
Alisema ni vyema Katibu Mkuu akajua kuwa amezungukwa na watu ambao wataendelea kumkwamisha kwenye utendaji wake kwa kuwa majibu yanayotolewa ni mepesi kwenye hoja za msingi.
Credit - Nipashe
No comments