Home
/
SIASA
/
WAPINZANI Waliibua Upya Sakata la Kivuko cha Magufuli Bungeni..Ni Kile Walichopewa JWTZ..!!!
WAPINZANI Waliibua Upya Sakata la Kivuko cha Magufuli Bungeni..Ni Kile Walichopewa JWTZ..!!!
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeibana Serikali kueleza kama Kivuko cha MV Dar es Salaam kilichosanifiwa na kutengenezwa kwa ajili ya kusafirisha abiria kinakidhi vigezo kwa matumizi ya kijeshi.
Kwa mujibu wa kambi hiyo, mwaka huu, Rais John Magufuli alitangaza kuwa kivuko hicho amekigawa kwa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kikosi cha Wanamaji.
Kivuko hicho hujulikana kama ‘Kivuko cha Magufuli’ kwa sababu kilinunuliwa wakati wa awamu ya nne alipokuwa Waziri wa Ujenzi kwa lengo la kuondoa tatizo la usafiri kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo.
Mbunge wa Momba, (Chadema), David Silinde alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akisoma maoni ya kambi ya upinzani kuhusu bajeti ya Wizara wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2017/18 kwa niaba ya Waziri Kivuli wa wizara hiyo, James Mbatia.
Silinde alisema kwa mujibu wa Kumbukumbu Rasmi za Bunge, Serikali ililiambia Bunge kuwa kivuko hicho hakikupokewa kwa sababu hakikuwa na vigezo vya kimkataba.
Alisema Serikali ilisema badala yake, kampuni iliyoiuzia Tanzania kivuko kile ilikuwa inakifanyia matengenezo ili kiweze kukidhi vigezo vya kimkataba likiwamo tatizo la ‘speed’ ambalo lilikuwa kinyume na matakwa ya kimkataba.
“Watanzania wanasubiri taarifa kama ukarabati wa kivuko kile umekamilika na kama kivuko kile sasa rasmi kimekabidhiwa kwa Serikali,” alisema na kuongeza:
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina tatizo na maamuzi hayo ya Rais ikiwa lengo la kugawa kivuko hicho ni kurahisisha ulinzi na ‘patrol’ (doria) katika eneo la Bahari ya Hindi ili kudhibiti magendo na uingizaji wa bidhaa haramu pamoja na wahamiaji haramu wanaotumia Pwani na fukwe za Bahari ya Hindi kuingia ndani ya nchi,” alisema.
Alihoji ni lini marekebisho ya kivuko hicho yalikamilika na ni lini kivuko hicho kilikabidhiwa kwa Serikali.
Silinde alisema bajeti ya kununua kivuko hicho ililenga kuondoa tatizo la usafiri kutoka Dar es Salaam hadi Bagamoyo mkoani Pwani.
Kambi hiyo ilihoji Serikali imetenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya kununua kivuko kingine ambacho kitafanya kazi ambayo ilikusudiwa kufanywa na MV Dar es Salaam.
Kuhusu ukata
Silinde alisema kitendo cha Serikali kushindwa kutekeleza bajeti katika kiwango kinachoridhisha ni matokeo ya vitendo vya Serikali kushindwa kutekeleza miradi ambayo imepangwa kutekelezwa na Serikali yenyewe.
“Huu ni udhaifu mkubwa kama mpangaji wa mipango ni wewe na wewe ndiye unashindwa kutoa fedha za utekelezaji, je, ni nani anatakiwa kutekeleza mipango hiyo? Hoja ni masuala yasiyokuwa kwenye mipango kupewa nafasi kubwa kuliko mipango iliyopangwa na kupitishwa na Bunge,” alisema.
Alisema kwa maneno mengine ni dharau kwa mhimili wa Bunge unaosimamia Serikali.
Silinde alisema fedha zilizotengwa katika mwaka wa fedha 2017/18 ni pungufu kwa Sh243.3 bilioni ukilinganisha na makadirio ya mpango wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2016/17.
“Vipaumbele vya miradi vitakavyotekelezwa ni miradi inayoendelea kutekelezwa, miradi inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo na miradi iliyopo kwenye Mpango wa Pili wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 hadi 2020/21.
Kambi hiyo iliishauri Serikali kuwa makini na kutekeleza vipaumbele kama ambavyo vimepangwa na kwamba kutotekelezwa maana yake ni kuwa Bunge lilitumia fedha na muda kama kivuli huku Serikali ikifahamu kuwa mpango huo hautekelezeki.
“Kambi rasmi ya upinzani inaona ipo haja ya kudurusu mpango huo kama unatekelezeka na pia haja ya kuwepo kwa sheria mahsusi ya kusimamia mpango huo,” alisema.
Vibali vya ujenzi
Silinde alisema kitendo cha mkuu wa nchi kutoa kibali kwa baadhi ya makandarasi bila kufuata taratibu za kutoa tenda (zabuni) kinaacha maswali mengi ya kujiuliza hata kama Rais alikuwa na nia njema.
“Lakini sasa wananchi lazima wajiulize kuhusu Serikali yao kuna masilahi gani na makandarasi waliopewa majukumu ya kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo? Je, umuhimu wa kuwa na sheria pamoja na taratibu za kusimamia tenda za Serikali umesitishwa au hautumiki tena?” alihoji Silinde.
Alitoa mfano wa fedha zilizopatikana baada ya sherehe za Mwenge kuamriwa kupelekwa kwenye ujenzi wa barabara ya Mwenge, ujenzi wa mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na ujenzi wa nyumba za Kota za Magomeni.
Silinde alisema hadi kufikia Februari mwaka huu makandarasi na wahandisi washauri walikuwa wanaidai Serikali takriban Sh788 bilioni ikilinganishwa na deni lililokuwapo Juni 30 mwaka jana la takribani Sh930 bilioni.
“Huu si utaratibu mzuri kwa Serikali kuendelea kuwakopa makandarasi ilhali wameshamaliza na kukamilisha wajibu wao wa kimkataba na kwa wale ambao hawajakamilisha miradi yao huongeza kasi ya utekelezaji kutokana na namna Serikali imekuwa ikitoa fedha kwao,” alisema.
No comments