Meli ya kijasusi ya Urusi yazama Uturuki..............
Meli ya kijasusi ya Urusi imezama baharini katika pwani ya Uturuki baada ya kugongana na meli ya kubeba mizigo, maafisa wa uchukuzi wa baharini wa Uturuki wamesema.
Wote waliokuwa kwenye meli hiyo wameokolewa.
Urusi awali ilikuwa imethibitisha kwamba meli ya Liman, ambayo ni sehemu ya kundi la meli za taifa hilo katika Bahari Nyeusi ilikuwa imepatwa na hitilafu na kwamba juhudi za kuizuia kuzama zilikuwa zinaendelea.
Chanzo cha kugongana kwa meli hizo hakijabainika lakini kulikuwa na ukungu mwingi eneo hilo.
Meli hiyo ya kijasusi iligonga meli yenye bendera ya Togo ambayo ilikuwa ikisafirisha mizigo, vyombo vya habari Uturuki vinasema.
Waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildirim amezungumza na mwenzake wa Urusi Dmitry Medvedev, na kumueleza masikitiko na huzuni yake kutokana na ajali hiyo, duru katika afisi ya waziri mkuu huyo wa Uturuki zimenukuliwa na shirika la habari la Reuters.
Kundi la Meli za Urusi Bahari Nyeusi (BSF) hupitia mlango wa bahari wa Bosphorus Strait kuelekea bahari ya Mediterranean, ambapo hushiriki katika harakati za kijeshi Syria.
Meli hiyo ya Urusi ilikuwa na watu 78 ambao waliokolewa wote.
Meli hiyo iligongana na meli ya Youzarsif H takriban 29km kutoka mji wa Kilyos kaskazini mwa mji wa Istanbul.
Haijabainika iwapo meli hiyo ilikuwa inaelekea mlango wa bahari wa Bosphorus wakati huo.
No comments